Nayo Lesotho inabaki kuwa nchi pekee ya Afrika ambayo hakuna mtu yoyote aliyeambukizwa na virus vya Corona hadi hivi sasa.
Rais Azali Assoumani, wa Comoros alitangaza Alhamisi asubuhi kwamba, kuna mtu mmoja mwenye umri wa miaka 50 anaeaminika aliambukizwa na Mkomoro mmoja aliyetokea Ufaransa Machi 18, na kulazwa hospitali April 23.
“Vipimo vyake hii leo vinathibitisha ana ugonjwa wa COVID 19. Hali yake ya afya inaendelea kuwa nzuri na sasa tunawatafuta wale wote waliokaribiana naye kufahamu jinsi alivyoambukizwa na watu ambao huenda waliambukizwa naye.” Amesema Rais Azali
Kutokana na hayo Rais Azali amesema anatangaza hatua za kupiga marufuku mkusanyiko wa zaidi ya watu 20, kufungwa shule na misikiti na amri ya kutotoka nje usiku.
Lakini wachambuzi na wananchi wengi wanasema serikali inaficha ukweli wa mambo kwani kuna watu wengi zaidi walioambukizwa na kuna watu wameshakufa na ugonjwa huo.
Mmoja wapo ni waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, akiwa mmoja wa wachache waliopigania uhuru wa Comoro, waliobaki, Muzawar abdallah alifariki Alhamisi asubuhi kutokana na kile familia yake inaiamabia Sauti ya Amerika kwamba, wameambiwa na madaktari kuwa ni dalili za COVID 19, lakini serikali haikuwaruhusu kutangaza.
Amri El-Arif Bobah, ambae ni binamu wa Abdallah amezungumza na Sauti ya Amerika na anasema hafahamu kwa nini serikali imechukuwa muda huu wote kutangaza kuwepo kwa ugonjwa huu wakati yeye anafahamu mjomba wake alikuwa ameambukizwa kulingana na madaktari.
“Mimi ninadhani uncle Mouzaoir, kafariki ndio, kwani tangu juzi alipelekwa hospitali kutokana na matatizo ya kisukari. Lakini hatimaye maradhi yake yamegeuka kuwa matatizo ya kupumua.” El-Arif anasema “serikali haitaki kukubali kwamba ugonjwa wa COVID-19 uko visiwani humo, hadi leo rais alipotangaza kuna mtu mmoja pekee yake.”
El-Arif anasisitiza kwamba “mimi bidhati ninaweza kukuambia uncle kafariki kutokana na ugonjwa huo wa COVID-19.”
Akizungumzia tangazo la Rais Azali la ikiwa kukiri kuwepo na mtu aliyembukizwa kutabadilisha hali ya mambo, El-Arif amesema “sidhani, unafahamu katika nchi inabidi serikali kutoa taarifa ya uhakika, ndipo watu watatanabahi kuna jambo, lakini ikisema kuna mtu mmoja pekee watu watadharau na kuendelea na maisha yao ya kawaida.”
Hilo ni jambo la hatari wanasema watalamu wa afya na kuitaka serikali ya Comoros kuchukuwa hatua kali zaidi za kudhibiti ugonjwa huo
Wakati huo huo inaripotiwa kwamba wafanyakazi wote wa huduma za afya katika hospitali kuu ya Al Maarouf wanakataa kuwahudumia wagonjwa kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujikinga.