Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:37

Marekani yatoa msaada wa $6.6 milioni kwa Kenya kupambana na Covid-19


Kituo cha Marekani cha Kutafiti na Kudhibiti Maradhi kimetangaza ufadhili wa shilingi milioni 705 kwa serikali ya Kenya kusaidia katika juhudi za kupambana na virusi vya Corona. 

Jumanne, serikali ya Marekani imetangaza ufadhili huu mpya kwa serikali ya Kenya kusaidia katika juhudi za kukabili maambukizi ya virusi vya Corona hasa katika mkakati wa kuzuia, kuitayarisha nchi na kutafuta suluhu kudhibiti maambukizi hayo na vile vile kuimarisha uwezo wa maabara kufanya vipimo vya juu vya afya.

Karibu wiki mbili zilizopita, Marekani kupitia shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa USAID lilitangaza ufadhili wa zaidi ya shilingi milioni hamsini kuwapa mafunzo wahudumu wa afya 700 katika majimbo 33 ya Kenya. Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa ufadhili huo ungeiwezesha serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kukinga wananchi wake kutokana na makali ya virusi vya Corona na vile vile kusaidia katika mwelekeo wa kuhamasisha umma kuhusu athari ya virusi hivyo hatari.

Katika ufadhili huu unaotarajiwa kupigia pondo shughuli za serikali ya Bw Kenyatta, Kituo cha Marekani cha Kutafiti na Kudhibiti Maradhi kinaeleza kuwa takriban shilingi milioni 180 zitawasilishwa mara moja kugharamia mahitaji ya kimsingi na muhimu kudhibiti virusi vya Corona nchini Kenya.

Pia, ufadhili huu utatumika kufanikisha manunuzi ya vifaa vya matibabu hasa kuwepo kwa vifaa vya upimaji wa sampuli za watu waliofanyiwa vipimo vya afya kubaini maambukizi ya virusi hivyo, kusaidia majimbo kadhaa kupanua uwezo wake wa kufuatilia ugonjwa huu na kuwawezesha wahudumu wa afya kujikinga dhidi ya maambukizi ya aina yoyote wakiwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa raia wa Kenya.

Alhamisi, wiki iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alifanya mazungumzo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, na kwa mujibu wa nyaraka za mawasiliano kutoka ikulu ya White House, Rais Trump alitoa ahadi kwa Bw Kenyatta kuwa Marekani itasaidia na kuunga juhudi za Kenya kupambana na janga hili. Katika mazungumzo hayo, Washington iliahidi kutoa msaaada zaidi kuiwezesha Nairobi kubuni na kuimarisha mkakati wake wa kukabili ueneaji zaidi wa virusi hivi.

Tangu Januari mwaka huu, kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa ubalozi wa Marekani nchini Kenya, Kituo cha Marekani cha Kutafiti na Kudhibiti Maradhi kimewatuma takriban wataalam wake 50 nchini Kenya kuunga juhudi za maafisa wa afya nchini kukabiliana na janga hili la Kimataifa. Wafanyakazi hawa wa CDC wanafanya kazi pamoja na maafisa wa afya wa Kenya katika maabara zake, ofisi za serikali za majimbo, na Kituo cha Operesheni na Afya ya Dharura Cha Umma kutoa mafunzo, ujuzi na kufuatilia mkondo wa maambukizi haya.

Hata havyo, wahudumu wa afya wiki hii nchini Kenya wametishia kugoma kulalamikia kukosekana kwa vifaa vya kujilinda wakiwa kazini, hali wanayoeleza kuwaweka katika hatari ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mpaka sasa Kenya imetangaza kushuhudia mafanikio makubwa katika juhudi zake za kukabili maambukizi ya virusi vya Corona hasa baada ya wagonjwa 124 kupata nafuu na kuachiliwa kuondoka hospitalini. Lakini pia katika kipindi hicho, Kenya imeripoti idadi jumla ya watu waliopata maambukizi haya kufikia 374 huku waliothibitishwa kufariki kutokana na virusi hivi hatari wakisalia 14.

-Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi.

XS
SM
MD
LG