Hisa kuu za soko la Australia S&P/ ASX 200 zimeuzwa kwa bei ya chini, na kuanguka kwa takriban asilimia 10 wakati wa kufunga mauzo hayo, wakati hisa za soko la Shanghai nchini China na hisa za Kospi Korea Kusini ziliporomoka kwa zaidi ya asilimia tatu na Hisa za Nikkei Japan zilimalizika kuuzwa kwa chini ya asilimia 2.5.
Hisa kuu za Hang Seng huko Hong Kong ziliporomoka kwa zaidi ya asilimia 4 wakati wa mauzo jioni.
Kuporomoka kwa hisa kuliendelea katika biashara ya asubuhi bara la Ulaya, ikiwa hisa za Uingereza FTSE na hisa za Frankfurt zote zikiuzwa kwa kiwango cha chini ya asilimia saba.
Uchumi wa dunia umekaribia kutokua wakati Marekani na serikali nyingine ulimwenguni zimetoa amri kwa raia wake kujiwekea karantini, ikifunga mashule, migahawa, saluni, vivutio vya utalii na burudani kudhibiti kuenea kwa kirusi COVID-19, ambacho kimewaathiri zaidi ya watu 169,00 duniani na kuuwa zaidi ya watu 6,500.
Benki Kuu ya Marekani imetangaza Jumamosi baada ya mkutano wa dharura kwamba itapunguza riba ili kufanya gharama za kukopa kuwa chini kusaidia biashara mbalimbali kuendelea ambapo janga kimataifa la corona limesababisha kudorora kwa uchumi.
Wakati huohuo Benki kuu ya Japan imerahisisha sera yake ya kifedha kwa kuimarisha ununuzi wa sarafu katika soko la fedha na mali nyingine zilizo katika hatari ya kufilisika.
Benki kuu ya Australia imeongeza pesa katika mfumo wake wa fedha unaopitia wakati mgumu, na kuahidi kutangaza hatua zaidi kunusuru uchumi wake.
Viongozi wa nchi saba tajiri zaidi duniani G7, wanatarajiwa kufanya mkutano kwa njia ya video hii Jumatatu, kujadiliana jinsi ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona.
Hatua zinazochukuliwa zinafanana na zile zilizochukuliwa mwongo mmoja uliopita wakati kulikuwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi kote duniani.
Imetayarishwa na waandishi wetu, Washington, DC.