Kesi ya madai imeanza kusikilizwa wiki hii katika mahakama ya serikali kuu ya Marekani katika mji wa Alexandria, Virginia dhidi ya Yusuf Abdi Ali, iliyofunguliwa dhidi yake na Farhan Mohamoud Tani Warfaa, anayesema kuwa aliteswa karibu ya kufa mwaka 1988 akiwa mikononi mwa Ali.
Kesi hiyo ya madai inaeleza kuwa Ali alikuwa kamanda wa Brigedia ya Tano ya Jeshi la Somalia, lililokuwa na jukumu la kulinda doria katika mkoa wa Somaliland uliojitenga. Inadaiwa kuwa Ali alimkamata Warfaa na vijana wengine mwishoni mwa mwaka 1987 ili wakahojiwe kufuatia kupotea kwa gari la kubeba maji.
Warfaa anasema kuwa aliwekwa kizuizini kwa miezi kadhaa, wakati ambapo alikuwa akivuliwa nguo na kubakia uchi na kupigwa. Katika mahojiano ya mwisho, Warfaa anasema, Ali alimpiga risasi mara kadhaa na kuwaamrisha askari kumzika, akiamini kuwa ameshakufa.
Lakini askari hao waligundua kuwa yuko hai na kumtorosha mpaka kwa familia yake wakibadishana naye kwa rushwa.
Ali alikimbilia Canada baada ya utawala wa Barre kuangushwa mwaka 1991. Aliletwa Marekani baada ya vitendo vyake vya jinai ya kivita kudhihirishwa katika Makala ya televisheni.
Amekuwa akiishi Virginia kwa zaidi ya miongo miwili, wakati fulani akifanya kazi ya ulinzi katika eneo la uwanja wa ndege iliyoko Washington. Wakili wake amekanusha tuhuma zote hizo.
Kesi hiyo imewasilishwa na kituo cha San Francisco kinachosimamia haki na uwajibikaji, ambacho kinapigania kuwaleta wote waliohusika na jinai za kivita mbele ya sheria.
Kesi kama hiyo pia ilipelekea hukumu ya malipo ya dola za Marekani milioni 21 dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Somalia Mohammed Al Samantar, ambaye pia anaishi Virginia baada ya utawala wa Barre kuanguka.