Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 12:52

Mwanajeshi wa Uganda ajiua baada ya kuua kiongozi wake, wenzake 2 Somalia


Wanajeshi wa Uganda wakiwa katika tukio maalum kabla ya kuanza shughuli za ulinzi wa amani chini ya Jeshi la Umoja wa Afrika (AMISOM), kabla ya kuondoka nchini Uganda kuelekea Mogadishu, Somalia, Aprili 12, 2018.
Wanajeshi wa Uganda wakiwa katika tukio maalum kabla ya kuanza shughuli za ulinzi wa amani chini ya Jeshi la Umoja wa Afrika (AMISOM), kabla ya kuondoka nchini Uganda kuelekea Mogadishu, Somalia, Aprili 12, 2018.

Uongozi wa jeshi la Uganda, wakishirikiana na uongozi wa kikosi cha wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia – AMISOM, wanachunguza tukio la mwanajeshi wa Uganda, aliyemuua kiongozi wake na wanajeshi wenzake wawili kabla ya kujiua.

Uganda inasema mwanajeshi huyo alifyatua risasi kiholela na kuua wenzake wote waliokuwa katika sehemu ya tukio, kikiwa kisa cha kwanza kwa mwanajeshi wa Uganda kuua wenzake wakiwa kazini, nje ya nchi.

Tukio hilo la Jumamosi, kwenye makao makuu ya Jeshi la Amisom nchini Somalia limetajwa na maafisa wa jeshi la Uganda kuwa la kushitukiza, bila kutoa sababu kamili wala kutaja majina ya wahusika, wakisema uchunguzi wa kina unaendelea.

Japo kuna taarifa kwamba afisa huyo wa jeshi alikuwa ameudhiwa na mkubwa wake, na kulikuwapo ukusiano mbaya wa kikazi kati yao, naibu msemaji wa Jeshi la Uganda UPDF Luteni Kanali Deo Akiiki amesema wachunguzi kutoka Uganda wamekwisha wasili Uganda na wameanza uchunguzi kwa kushirikiana na uongozi wa Amisom.

“Tunapeleleza kilichosababisha tukio hilo. Tumetuma wapelelezi watakaoshirikiana na uongozi wa Amisom nchini Somalia na watakapotupatia ripoti, tutajua sababu kamili”, amesema Deo Akiiki, naibu wa msemaji wa jeshi la Uganda UPDF

Hili ni tukio la kwanza kwa mwanajeshi wa Uganda kuua kiongozi wake. Ni mara ya kwanza pia kwa mwanajeshi wa Uganda kushambulia wenzake na kuwaua wakiwa nje ya nchi kazini.

Matukio ya wanajeshi wa Uganda kuua raia au wenzao kufuatia mzozo wa kifamilia, mapenzi, umiliki wa mali, sababu zisizojulikana ni kawaida nchini Uganda.

Mwaka 2018, mwanajeshi Isaac Okello alihukumiwa kifungo cha miaka 80 kwa kumuua mama mjamzito, mumewe na mtoto wao wa kiume katika wilaya ya Alebtong, kaskazini mwa Uganda.

Mwaka 2016, Sagenti Isaac Obua, aliua wanajeshi wenzake saba katika kambi ya Makindye jijini Kampala.

Mwaka 2018 mwanajeshi Patrick Odoch alihukumiwa miaka 90 gerezani na mahakama ya kijeshi, baada ya kuua raia 11 karibu na makao makuu ya kambi ya jeshi ya Bombo.

Hivi vikiwa ni visa vichache tu kati ya vingi, vya wanajeshi wa Uganda kutekeleza mauaji kinyume cha sheria. Lakini naibu wa msemaji wa jeshi Deo Akiiki, anasema huenda sababu zisiwe zinakaribiana na tukio la Jumamosi nchini Somalia.

“Japo wanajeshi wamekuwa wakiua raia Uganda na hata kuua wenzao kwa kuwapiga risasi, halijawahi kutokea nje ya nchi kama hili la Somalia. Tuna matumaini kwamba wapelelezi watatupatia taarifa kamili,” ameongeza kusema Akiiki.

Jeshi la Uganda vile vile limekanusha baadhi ya taarifa kwamba huenda mazingira ya kazi kwa wanajeshi nchini Somalia ni magumu.

“Sitegemei kwamba kazi ni ngunu nchini Somalia kwa sasa. Kazi ilikuwa ngumu mwanzoni, tulipowasili nchini humo. Wanjeshi wetu hupewa likizo. Kwa hivyo sidhani mwanajeshi huyo alikuwa na msongo wa mawazo au labda alikuwa anapata wakati mgumu kazini” amesema Akiiki.

Uganda ndio ilikuwa ya kwanza kutuma wanajeshi wake nchini Somalia kupambana na wanamgambo wa Al-shabaab na ndiyo yenye idadi kubwa ya wanajeshi. nchi nyingine ni Kenya, Burundi, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington DC.

XS
SM
MD
LG