Zelenskyy asema hakuna anayeweza kutabiri vita vitamalizika lini

Volodymyr Zelenskyy

“Hivi leo hakuna anayeweza kutabiri vita hivi vitaendelea kwa muda gani,” Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema Ijumaa katika hotuba yake anayoitoa kila siku kuhusiana na uvamizi wa Russia huko Ukraine.

“Lakini tunafanya kila tunachoweza kuikomboa haraka ardhi yetu. Hiki ni kipaumbele chetu – kushughulika kila siku kufanya vita hivi viwe vifupi,” alisema.

Zelenskyy alisema urefu wa vita “utategemea, kwa bahati mbaya, siyo tu kwa watu wetu, ambao tayari wanafanya juhudi kwa uwezo wao wote.”

Alisema, “Pia inategemea na washirika wetu- nchi za Ulaya, kwa nchi hizi za ulimwengu wote huru.”

Uwezekano wa kupanuka kwa NATO, kufuatia mzozo uliojitokeza nchini Ukraine, itakuwa ndiyo lengo la mazungumzo ya Jumamosi, wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akielekea Berlin kwa ajili ya mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO.

Rais wa Finland Sauli Niinisto na Waziri Mkuu Sanna Marin wameelezea kuunga mkono kwao kujiunga na muungano huo, hatua ambayo itakamilisha mabadiliko makubwa ya sera kwa Scandinavia ikiwa ni majibu kwa uvamizi wa Russia huko Ukraine.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema Ijumaa nchi yake haiungi mkono Finland na Sweden kujiunga na NATO, akielezea uungaji mkono wao wa kile Uturuki inakadiria ni taasisi za kigaidi, kama vile vikundi vya wanamgambo wa Kikurdi.

“Tunafuatilia matokeo haya kuhusu Sweden na Finland, lakini sisi hatupendelei wazo hili,” Erdogan aliwaambia waandishi wa habari mjini Istanbul. Kwa namna yoyote ya kuongezeka wanachama wa NATO kunahitaji makubaliano ya pamoja ya nchi wanachama.

Msimamo wa Marekani

Maafisa wa Marekani walisema wanafuatilia “kupata ufafanuzi wa msimamo wa Uturuki,” wakati wakisisitiza kuwa “Marekani itaunga mkono maombi ya Finland na /au Sweden iwapo wataamua kuomba kujiunga.”

“Tunaunga mkono kwa nguvu zote sera ya Uwazi ya NATO,” Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Masuala Ulaya na Eurasia Karen Donfried aliwaambia waandishi Ijumaa.

“Nafikiri hilo ni muhimu kukumbuka kuwa nguzo za msingi za Marekani ni kutetea katika misingi ya msaada wake kwa Ukraine kuwa ni haki ya kila taifa huru kuamua mustakbali wake wa mpangilio wa sera za nje na usalama.”