Marekani : Wizara ya Ulinzi, idara ya Posta zapata fedha baada ya serikali kufungwa

Kutoka kushoto : Kiongozi wa walio wachache Nancy Pelosi, Makamu wa Rais Mike Pence, Rais Donald Trump na Kiongozi wa walio wachache katika Baraza la Seneti Chuck Schumer wakiwa katika mazungumzo ya kuepusha serikali kufungwa ambayo yaligonga ukuta, Jumanne, Disemba 11, 2018.

Kufuatia mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na viongozi wa bunge la Congress, baadhi ya ofisi za serikali ya Marekani zilifungwa kuanzia Jumamosi baada ya mazungumzo kushindwa kufikia makubaliano ya kuendelea kuipatia fedha serikali kuendesha shughuli zake kikamilifu.

Takriban idadi kubwa ya wakala na idara za serikali, zikiwemo Wizara ya Ulinzi na nyengine ni Huduma za Posta, tayari zimepatiwa fedha na zitaendelea na operesheni zake za kila siku.

Lakini wafanyakazi 800,000 wa Idara ya Ulinzi wa Ndani, Usafiri na idara nyingine zimeathiriwa na kufungwa kwa serikali.

Kwa mujibu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Serikali ya Marekani, watu 420,000 ambao wanatambulika kuwa ni “muhimu” itawalazimu kufanya kazi bila ya malipo, wakati watu wengine 380,000 hawataweza kuripoti kazini kabisa.

Maafisa wa utawala waTrump wanasema yeyote anaye lazimika kufanya kazi bila ya malipo watalipwa mara tu makubaliano yatakapo fikiwa.