WHO yaahidi dozi milioni 220 za chanjo ya COVID-19 kwa Afrika

FILE -Majaribio ya chanjo ya COVID-19 inayoendelea kufanyiwa uchunguzi na Mashirika ya Afya ya Taifa na Moderna Inc. hubo Binghamton, New York, July 27, 2020.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema nchi za Afrika zitapewa dozi milioni 220 za chanjo ya virusi vya Corona punde tu chanjo hiyo itakapoidhinishwa.

Chanjo ya kwanza itatolewa kipaumbele kwa wafanyakazi walio mstari wa mbele kupambana na janga la Corona na makundi yaliyoko hatarini kiafya.

Kulingana na afisa wa mipango wa shirika la afya duniani barani Afrika Richard Mihigo, utoaji wa chanjo hiyo utazingatia idadi ya watu katika kila nchi.

Vyanzo vya habari vimeeleza Mihigo amesema kwamba nchi 54 zimeeleza nia ya kutaka chanjo dhidi ya virusi vya Corona. Afrika ina jumla ya watu bilioni 1.3.

Taarifa zaidi zinaeleza nchi 54 barani humo zimeeleza wanataka chanjo ya Covid-19.

Habari zaidi zinasema programu inayofahamika kama COVAX, inakusudia kusaidia kununua na kusambaza kwa usawa dozi bilioni mbili za chanjo zilizoidhinishwa ifikapo mwisho wa mwaka 2021.

Mpaka sasa ziko chanjo tisa ambazo zinafanyiwa majaribio duniani mbili kati ya hizo zinafanyiwa majaribio Afrika.