Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:14

India yaweka rekodi ya maambukizi ya juu zaidi duniani katika saa 24


Waendesha pikipiki wakivalia vifaa vya kujilinda na Covid-19, wakipita ndani ya soko la New Delhi Agosti 30, 2020.
Waendesha pikipiki wakivalia vifaa vya kujilinda na Covid-19, wakipita ndani ya soko la New Delhi Agosti 30, 2020.

India imeripoti maambukizi mapya ya virusi vya corona 78,761 katika kipindi cha saa 24 Jumapili, ikiwa ni idadi ya juu kabisa katika ongezeko la siku moja duniani tangu janga hili kuanza, wakati nchi hiyo ikiendelea kufungua uchumi wake.

Hii ilikuwa siku ya nne mfululizo ambapo India imesajili zaidi ya maambukizi 75,000.

Ikiwa na idadi ya watu bilioni 1.4, India ni nchi ya tatu yenye maambukizi ya juu kabisa duniani, ikiongozwa na Marekani na Brazil, ikiwa na maambukizi milioni 3.5 na vifo zaidi ya 63,000, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya nchi hiyo.

Katika miji kadhaa ya Ulaya Jumamosi waandamanaji walikusanyika wakikiuka masharti yaliyowekwa tangu mlipuko wa COVID-19 kuanza.

Maelfu ya waandamanaji walijitokeza katika mitaa ya Berlin kuandamana dhidi ya amri ya kuvaa barakoa na kutokaribiana. Polisi wanasema wamewakamata waandamanaji takriban 300.

Huko London, waandamanaji katika viwanja vya Trafalgar Square walikusanyika kupinga kile walichokiita ni “ukandamizaji wa kitiba” ukiwalazimisha kuvaa barakoa na kutokaribiana.

Mamia kadhaa ya waandamanaji mjini Paris waliandamana dhidi ya sheria ya mji mkuu huo ya kuwalazimisha watu kuvaa barakoa.

Mjini Zurich, waandamanaji wapatao 1,000 wakitilia mashaka kanuni zilizowekwa kudhibiti COVID-19 walidai “kurejeshwa kwa uhuru.”

Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani kinaripoti kuwa kuna zaidi ya maambukizi milioni 25 ya COVID-19 duniani. Marekani inakaribia kufikia maambukizi milioni 6, ikufuatiwa na Brazil yenye maambukizi milioni 3.8 na India maambukizi milioni 3.5.

End

XS
SM
MD
LG