Katika tukio hilo lililotokea usiku wa Jumapili, maji ya mto yalizisomba wilaya za Derna, mji ulioko mashariki mwa Libya, baada ya mabwawa mawili kupasuka. Maelfu waliuawa na maelfu wengine hawajulikani walipo.
Umoja wa Mataifa ulizindua ombi la msaada wa zaidi ya dola milioni 71 kuwasaidia maelfu ya watu wenye shida na kuonya "kiwango cha tatizo" bado hakijafahamika.
Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa alisema siku ya Ijumaa kuwa Libya inahitaji vifaa vya kuwatafuta watu waliokwama kwenye matope na majengo yaliyoharibiwa pamoja na huduma za afya za msingi ili kuzuia a mlipuko wa kipindupindu miongoni mwa walionusurika.
"Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni makazi, chakula, huduma muhimu za matibabu kwa sababu ya wasiwasi wa kipindupindu, wasiwasi wa ukosefu wa maji safi," Martin Griffiths aliuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Alisema ofisi ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetuma timu ya watu 15 kwenda Libya kuratibu wa maafa. Timu hiyo ilikuwa nchini Morocco ambako ilikuwa ikiratibu tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo wiki iliyopita.
Eneo la Derna, ni kitovu cha uharibifu mashariki mwa nchi hiyo , liliangamizwa na mafuriko ambayo yaliangusha majengo yote wakati familia zikiwa zimelala.
Griffiths amesema pendekezo lililotolewa na meya wa Derna la
kuunda ukanda wa bahari ili kupeleka misaada linaweza kuwa njia bora mbadala, ikizingatiwa kuwa mji huo uko kwenye Bahari ya Mediteranian.
Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika mengine ya misaada siku ya Ijumaa yalitoa wito kwa mamlaka nchini Libya kusitisha kuwazika waathirika wa mafuriko katika makaburi ya pamoja, kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa inayoonyesha kuwa hadi sasa zaidi ya watu 1,000 wamezikwa kwa namna hiyo tangu nchi hiyo ikumbwe na mafuriko.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP na Reuters.