Wanne wauawa wakati maandamano dhidi ya mapinduzi yakiendelea Myanmar

Dada wa mmoja wa waandamanaji aliyeuawa wakati wa maandamano (wapili kushoto) mwili wake ukipelekwa katika kituo cha afya cha muda huko Mandalay, Myanmar, March 13, 2021.

Waandamanaji walijitokeza mitaani nchini Myanmar kwa mara nyingine Jumamosi na vikosi vya usalama vilijibu kwa kufyatua risasi kwa makundi ya waandamanaji. Kiasi cha waandamanaji wanne walifariki huko Mandalay, mji wa pili kwa ukubwa, na mji wa kati wa Pyay. 

Wakati maandamano na ghasia zikiendelea huko Myanmar, mchunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar ameitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua msimamo wa pamoja dhidi ya utawala wa kijeshi uliofanya mapinduzi Februari 1 na kuingia madarakani.

“Inavunja moyo kushuhudia hofu na uvunjifu wa amani unaofanywa na wale waliojichukulia madaraka kwa nguvu huko Myanmar,” ambayo pia inajulikana kama Burma. Thomas Andrews ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la UN Ijumaa.

Thomas Andrews

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa “lazima ichukue hatua dhidi ya utawala wa kijeshi ambao hauna khofu ya kushtakiwa.

Afisa mmoja wa Myanmar ameliambia baraza hilo kuwa mamlaka nchini humo “zinajizuilia vya kutosha” katika kukabiliana na waandamanaji.

Andrews ameyaita madai hayo “ni upuuzi.”

Tangu jeshi la Myanmar kukamata madaraka kwa nguvu kutoka kwa serikali iliyochaguliwa na wananchi, amesema, majeshi ya usalama yamewaua watu wasiopungua 70 na kuwakamata kiholela zaidi ya watu 2,000.

Andrews pia amesema kuna ushahidi wa picha za video zinazoonyesha wanajeshi wakiwapiga kinyama waandamanaji, kuharibu mali, kuiba katika maduka, na kufyatua risasi kiholela katika nyumba za watu, na kuwa utawala wa kijeshi umekuwa ukiharibu sheria zinazowalinda raia na kukandamiza uhuru wa kujielezea na kukusanyika.

Mwezi uliopita serikali ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi Burma.

Min Aung Hlaing

Mapema wiki hii, Serikali ya Marekani iliweka vikwazo dhidi ya watoto wawili wakubwa wa mkuu wa jeshi la Burma Min Aung Hlaing.

Marekani imetoa wito wa kuachiliwa mara moja Aung San Suu Kyi, kiongozi wa Chama cha National League for Democracy, Rais Win Myint aliyeondolewa madarakani, waandamanaji, waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu ambao wamewekwa kizuizini bila ya haki tangu utawala wa jeshi kufanya mapinduzi.

Aung San Suu Kyi