Ilikuwa saa mbili asubuhi huko Adre, Chad, mji ulio katika mpaka na Sudan. Raia wa Chad wanarejea kutoka Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, ambao baadhi ya watalaamu wanasema umekumbwa na mapigano makali sana kuliko mji mkuu wa Sudan, Khartoum katika wiki za karibuni.
Mmoja wa wale waliorejea amezungumza na VOA mara tu baada ya kuvuka mpaka kutoka Sudan. Ameomba asitajwe jina lake ili kulinda usalama wa familia yake.
“Ilianza mwanzoni mwa mwezi wa Ramadhan. Matatizo mengi. Walichoma nyumba na kuua watu pia. Wengi sana. Kwanza, walikuwa nje ya mji, lakini halafu walifika katika ujirani ndani ya mji. Waliiba sokoni. Walivunja kila kitu, hasa katika maduka na masoko. Walichukua kila kitu,” anasema mama huyu mkimbizi kutoka Darfur Magharibi.
Wale waliorejea wanasema walikimbia kwa kujificha nyakati giza lilipoingia ili kuepuka kupigwa risasi. Haiko bayana ni kundi gani kati ya hayo yanayopigana nchini Sudan lilifanya uharibifu huo.
Muda mfupi baadaye, mikokoteni ya farasi iliyowabeba wakimbizi wa Sudan waliokimbia Geneina iliwasili.
Mkimbizi wa Sudan Abdel Ennaser Abdallah Adam alielezea jinsi mji huo ulivyoathiriwa na mapigano.
“Yote hayo. Walichoma kambi za jeshi. Hakuna kilichobaki. Kila kitu kiliharibiwa na kuibwa. Nina maana, majengo yote hivi sasa mjini humo yameharibiwa. Kuanzia mahospitali, vituo vya polisi, mashule, kila kitu,” anasema Abdallah Adam.
Mapigano kati ya majeshi ya Sudan na kikosi maalum cha Rapid Support Forces, ambayo yameonyeshwa kwenye kanda ya video yanaonyesha hali ilivyokuwa na mji ulivyoharibiwa.
Bado haijulikani watu wangai wameuawa huko Geneina tangu mapigano yalipoanza.
Tangu Mei 19, mitandao ya simu za mkononi mjini humo imeacha kufanya kazi kabisa, na kupelekea watu wengi kuwa na wasi wasi kuhusu hatima ya jamaa zao na washirika wao ambao bado wako huko.
Mathilde Vu, wa Baraza la Wakimbizi la Norway, alisema kundi la misaada linakhofia mambo yatakuwa mabaya sana kwa wenzao walioko mjini humo.
Mathilde Vu anasema “kwa mfano, tumeona viwango vya juu mno vya ghasia katika mwezi huu. Kumekuwepo mashambulizi kadhaa. Kwa hakika kuna hali ya ghasia kila mahali, katikati ya mji, maeneo ya makazi ya watu yanapigwa makombora na walenga shabaha wanawalenga watu. Kambi za wasiokuwa na makazi zimechomwa, na watu wengi wamelazimika kukimbia sehemu nyingine mjini humo, lakini hakuna sehemu ambayo ni salama.”
Idadi ya watu huko Geneina ilikuwa kiasi cha laki mbili na nusu, lakini maelfu wamekimbilia kwenye maeneo ya wakimbizi nchini Chad kama Borota. Wakimbizi wanasema ni hatari sana kuondoka mjini humo na hatari sana pia kubaki, kwahiyo watu wengi kwa kweli hawafahamu nini cha kufanya.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC inasema hali ya kibinadamu ni mbaya sana.
Msemaji wa ICRC, Alyona Synenko anaelezea zaidi. “Fursa ya upatikanaji chakula inazidi kuwa ngumu. Kiasi cha watu milioni 3 wamekoseshwa makazi kabla hata ya mzozo kuanza. Kwahiyo, watu, wamepitia mambo mengi na ustahmilivu wao umedhoofishwa na changamoto hizo mbali mbali, hivi sasa wanakabiliwa na duru mpya ya ghasia ambapo wamekimbia tena kutoka kwenye nyumba zao.”
Wasudan wengi wanaoangalia kwenye mitandao ya kijamii wanalalamika kwamba vyombo vya habari vimelenga kwa kiasi kikubwa mapigano ya huko Khartoum, na kutoa mtizamo mdogo kwa mapigano ya huko Darfur Magharibi.
Imetayarishwa na Henry Wilkins, VOA Adre, Chad