Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 21:07

Mgao wa Chakula kwa wakimbizi Tanzania


Mtoto Kevin, ambaye ni mkimbizi akiulamba mkono wake akifurahia chakula huko Nyabitara Transit, Burundi. Tarehe 3 Oktoba 2019. Picha na TCHANDROU NITANGA / AFP.
Mtoto Kevin, ambaye ni mkimbizi akiulamba mkono wake akifurahia chakula huko Nyabitara Transit, Burundi. Tarehe 3 Oktoba 2019. Picha na TCHANDROU NITANGA / AFP.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema Jumanne kwamba zaidi ya wakimbizi 200,000 nchini Tanzania watapokea nusu tu ya mgao wa chakula kuanzia mwezi ujao kwa sababu ya ukosefu wa ufadhili wa kifedha.

Ikiwa ni mara ya pili katika miezi ya hivi karibuni kwa Tanzania kupunguziwa mgao huo, imeingia katika mkumbo wa nchi nyingine duniani ambazo shirika la Umoja wa Mataifa la chakula zimewapunguzia mgao wa chakula kwasababu ya kukabiliwa na upungufu wa fedha taslimu na kupanda kwa bei ya vyakula kutokana na vita nchini Ukraine.

Mgao wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Tanzania -- ambao asilimia 70 wanatokea Burundi na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – umekuwa ukipungua taratibu tangu mwaka 2020, WFP ilisema katika taarifa.

Mwezi Machi, migao hii, iliyopangwa kukidhi kiwango cha chini kilichopendekezwa cha kilokalori 2,100 kwa kila mtu kwa siku, ulipunguzwa kutoka asilimia 80 ya kiwango hicho hadi asilimia 65.

"Mwezi Juni, mgao huo utashuka zaidi hadi asilimia 50, ambayo inaweza kuwaacha maelfu ya wakimbizi wakihangaika kukidhi mahitaji yao ya lishe," WFP ilisema, na kuongeza kuwa dola milioni 21 zinahitajika haraka ili kuepuka kupunguzwa zaidi.

Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Tanzania, Sarah Gordon-Gibson, alisema: "WFP ina wasiwasi mkubwa kwamba upunguzaji mkubwa utawalazimisha wakimbizi kuingia katika mazingira magumu zaidi."

WFP ilitangaza mwezi Machi kuwa mgao wa chakula pia utakatwa kwa wakimbizi nchini Burundi na Bangladesh, na kuomba ufadhili wa dharura ili kuepuka Yemen kupunguziwa zaidi.

Shirika hilo pia limepunguza mgao katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni ktokana na matatizo ya muda mrefu ya ufadhili, ikiwa pamoja na maeneo yaliyokumbwa na maafa ya Ethiopia, Sudan Kusini na Kenya.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.

Forum

XS
SM
MD
LG