Akizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu siku ya Alhamisi, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Wakimbizi Tanzania, Sudi Mwakibasi amesema, hivi sasa watu wote walioingia nchini humo kwa lengo la kuomba hifadhi ya ukimbizi wamepokelewa na kuwekwa Kigoma mjini wakisubiri taratibu zikamilike kabla ya kupelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
“Kamati ya kitaifa ya kuhoji wakimbizi, itawahoji waombaji wote wa hifadhi na kisha itawachuja, na wale wenye vigezo vya ukimbizi watapekekwa kambini” alisema Mwakibasa.
Tanzania inapokea na kuwahudumia wakimbizi kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa Geneva. Alisema Mkurugenzi huyo.
Kulingana na taarifa zilizochapishwa na gazeti la The East African siku ya Alhamisi, zaidi ya watu 2,600, wengi wao watoto, wanawake na wazee, wamekuwa wakikimbilia Tanzania tangu mwanzoni mwa mwezi Machi.
Taarifa hiyo imesema raia hao wa DRC wamekuwa wakiingia nchini katika makundi madogo madogo yenye watu kati ya 300 mpaka 600.
Shirika la habari la AFP limeripoti kushindwa kwa juhudi nyingine za usitishaji mapigano huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa kufanywa mazungumzo ambayo hakuna upande unaoonekana unataka kushiriki, wakati majeshi ya nje yakiendelea kuingia.
Mbali na juhudi kubwa za kidiplomasia za kusitisha mapigano kuna fursa ndogo ya kukomesha uasi mpya huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika siku za karibuni.