Wairan waendelea kupinga uongozi wa kidini kwa maandamano na migomo

FILE - Pikipiki ya polisi ikiwaka moto wakati wa maandamano kulaani kifo cha Mahsa Amini, Tehran, Iran Sept. 19, 2022. (West Asia News Agency via Reuters)

Wairan wakiwa na hasira juu ya  kifo cha msichana aliyekuwa chini ya ulinzi wa  polisi walionyesha ushujaa kwa kukabiliana na risasi na gesi ya kutoa machozi siku ya Jumamosi.

Hayo yameelezwa na kikundi cha haki za binadamu, kikisema wananchi wameendeleza maandamano dhidi ya watawala wa kidini ambao wanakabiliwa na upinzani mkubwa wa umma.

Ripoti ya uchunguzi wa maiti nchini Iran imekanusha kwamba Mahsa Amini alifariki kutokana na kipigo cha kichwani na katika viungo vya mwili wakati akiwa anashikiliwa polisi na kukihusisha kifo chake na matatizo ya kiafya aliyokuwa nao, vyombo vya habari vya serikali vilisema Ijumaa.

Kifo cha Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22, ambaye ni Muiran Mkurdi, kilichochea maandamano nchi nzima, ikiwa changamoto kubwa sana kwa viongozi wa kidini wa Iran ambao wamekuwepo madarakani kwa miaka kadhaa.

Wanawake walivua mitandio yao wakikaidi amri ya utawala wa kidini wakati umati wenye hasira ulipaza sauti wakiutaka utawala wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei uangushwe.

Baada ya wito wa maandamano makubwa ya umma Jumamosi, majeshi ya usalama waliwafyatulia risasi waandamanaji na kutumia gesi ya kutoa machozi katika miji ya Kikurdi ya Sanandaj na Saqqez, kulingana na kundi la Iran la haki za binadamu la Hengaw.

Migomo imesambaa kote katika miji ya Saqqez, Diwandareh, Mahabad na Sanandaj, alisema Hengaw.

Moja ya shule zilizopo katika uwanja wa jiji la Saqqez ulikuwa umejaa wasichana wa shule waliokuwa wakipiga kelele “mwanamke, uhai, uhuru,” kikundi cha haki za binadamu kilisema.

Hengaw ilisema Jumamosi kuwa majeshi ya usalama ya Iran yalikuwa yameanzisha msako katika miji miwili ya kikurdi.

“Majeshi ya usalama yanafyatua risasi kwa waandamanaji katika miji ya Sanandaj na Saqqez,” ilisema Hengaw. Ilisema askari wa kutuliza ghasia walikuwa wanatumia mabomu ya kutoa machozi.

Akaunti ya Twitter ya Tavsir1500 ambayo inafuatiliwa sana imeripoti ufyatuaji wa risasi kwa waandamanaji katika miji miwili ya Kikurdi ya kaskazini magharibi.

Makundi ya haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 150 wameuawa, mamia wamejeruhiwa na maelfu wamekamatwa na majeshi ya usalama yanayokabiliana na waandamanaji.

Amini alikamatwa mjini Tehran Septemba 13 kwa kuvaa “vazi lisilokubalika,” na alifariki siku tatu baadae.

Serikali imeeleza kuwa maandamano ni njama ya maadui wa Iran ikiwemo Marekani, ikiwashutumu waasi wenye silaha – kati ya wengine – kusababisha uvunjifu wa amani ambapo takriban wanajeshi 20 wa vikosi vya usalama wameripotiwa kuuwawa.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.