Wagombea walijaribu kila mmoja kujiweka kando na mgombea ambaye anaongoza katika kinyang’anyiro hicho rais wa zamani Donald Trump na masuala kadhaa ya kimataifa.
Mdahalo wa tatu wa wagombea urais wa chama cha Republican, uliorushwa na kituo cha televisheni cha NBC, ulijikita zaidi katika sera ya mambo ya nje.
Wakizungumzia mzozo wa Israel na Hamas, Mgombea urais wa Chama cha Republican Gavana Ron DeSantis, angemueleza Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuwa “Imalize hiyo kazi kabisa kwa hawa wachinjaji, Hamas. Ni magaidi. Wanaua raia wasiokuwa na hatia; watawatokomeza wayahudi wote kwenye hii dunia kama wanaweza.”
Naye Seneta Tim Scott, alisema “Huwezi kufanya mashauriano na muovu. Lazima ummalize kabisa.”
Wakati Nikki Haley, alisema “Hakuna Hamas bila ya Iran. Hakuna Hezbollah bila ya Iran. Hakuna Wahouthi bila ya Iran.”
“Nani anaifadhili Iran hivi sasa? China inanunya mafuta kutoka iran. Russia inapata drones na makombora kutoka Iran na kuna muungano usio mtakatifu,” Alisema Haley.
Huku kukiwa na wagombea watano ambao wameshiriki katika mdahalo, kila mmoja alikuwa na muda wa ziada kuzungumza kuliko ilivyokuwa katika midahalo iliyopita.
Kuhusu fedha zaidi kwa Ukraine – kulikuwa na baadhi ya mgawanyiko.
Chris Christie, alisema “Haya ni maamuzi. Hii ni gharama tunayolipa kwa kuwa viongozi wa dunia huru.”
Wakati Vivek Ramaswamy alisema “Ukraine si mfano wa demokrasia. Hii ni nchi ambayo ilivipiga marufuku vyama 11 vya upinzani. Imekamata fani ya habari kwa kua na kituo kimoja cha televisheni cha serikali. Hii si demokrasia.”
Naye Chris Christie, alisema “Sote tunakumbuka kile ambacho yule mhuni ambaye alivamia Ukraine. Sote tunafahamu kwamba watu nusu milioni wamefariki kwasababu ya Putin.”
“Hapa tunapenda uhuru, nchi inayoiunga mkono Marekani ambayo inapigania kujinusuru na demokrasia yake,” aliongeza.
Huku fentanyl ikiwa kupitia kwenye mipaka ya kusini mwa Marekani, DeSantis alisema atakwenda ndani zaidi kuliko kile ambacho alifanya Donald Trump wakati wa urais wake.
“Pia nitajenga ukuta mpakani na kuitaka Mexico ilipie kama alivyoahidi Donald Trump. Utafanya vipi? Mexico haitatoa fedha. Tutaweka ada maalum kwa ajili ya fedha ambazo wafanyakazi wa kigeni wanatuma katika nchi zao. Tutachangisha mabilioni ya dola. Nitajenga ukuta.” Alisema Gavana Ron DeSantis.
Wakati huo huo rais wa zamani, Donald Trump alifanya wake kiasi cha kilometa 16 katika eneo la Hialeah, Florida, mkutano uliohudhuriwa na kundi kubwa la jamii ya Wahispania.
Akizungumza na Sauti ya Amerika Jennifer Lawless, Mwenyekiti wa Idara ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Virginia, anasema wagombea hawa hawatakuwa wazuri zaidi ya Trump katika kura za maoni.
Lawless alisema “Huku Donald Trump akiwa na zaidi ya asilimia 50 ya kura za maoni na akiwa juu kwa asilimia 40 kwa wengine wengi, hakuna mgombea hata mmoja aliyemkaribia katika nafasi ya pili.”
Hata hivyo alisema “Lakini kama kuna kitu kitatokea, Donald Trump ama awe gerezani au ashindwe kuwania urais au alazimishwe kuachia ngazi kuingia katika ushindani, kwa sababu mbali mbali za kisheria, yeyote atakayekuwa katika nafasi ya pili ndiyo atakuwa na fursa nzuri.” Muda unazidi kuyoyoma.
Wapiga kura watamchagua rais mpya katika kipindi cha mwaka mmoja tu. Na mkutano wa kwanza wa wagombea urais utafanyika miezi michache ijayo.