Wademokrat wanamaliza kutoa hoja Ijumaa, wafafanua 'makosa' ya Rais Trump

Rais Trump

Timu ya wabunge ya Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani, wanamaliza kutoa hoja zao za ufunguzi Ijumaa, baada ya kufafanua kwa undani jana, sababu za kumshtaki rais kutokana na utumiaji mbaya wa madaraka na kuzuia bunge kufanya kazi yake.

Katika siku ya pili ya kutoa hoja ya ufunguzi, waendesha mashtaka, ambao ni wabunge wa chama cha Demokrat wameeleza kwamba, Trump alizuia msaada wa kijeshi ulioidhinishwa na bunge kwa ajili ya Ukraine kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa, wakisisitiza ni kosa baya kabisa.

Wademokrat wanasisitiza dhana kwamba Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden alihusika katika ulaji rushwa nchini Ukraine pamoja na kijana wake haitahitaji wao kutoa ushahidi mbele ya baraza hilo jinsi vile WarepubliKan wanavyotaka.

Siku ya Ijumaa timu ya waendesha mashtaka wataeleza kwa kina jinsi Rais Trump alivyozuia baraza la wawakilishi kufanya kazi zake kwa kuwazuia washauri wake wa karibu kutotoa ushahidi wala kuwasilisha nyaraka zote zinazohusiana na kesi hiyo.

Hapo Kesho itakuwa ni zamu ya mawakili wa Rais Trump kutoa hoja zao kupinga mashtaka hayo kwa siku tatu.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC