Kesi hiyo inatokana na mashtaka mawili yaliyofikishwa mbele ya seneti kuhusiana na kadhia ya Ukraine ambapo inadaiwa Rais Trump alitumia vibaya madaraka yake kwa kuzuia msaada wa kijeshi kwenda Ukraine.
Inadaiwa Trump alikuwa anaishinikiza Ukraine kuanzisha uchunguzi dhidi ya mpinzani wake wa kisiasa Joe Biden iwapo wanataka msaada huo uwafikie.
Pia inadaiwa kuwa Trump alizuia mkondo wa sheria wa bunge kufanya kazi yake.
Kesi hiyo inaendelea hii leo baada ya mjadala wa zaidi ya saa 12 Jumanne, ulomalizika saa nane usiku ambapo maseneta waliidhinisha kanuni za kuendesha kesi hiyo kwa kura 53 kwa 47.
Kura hiyo ilifuatia majadiliano ya kujaribu kubadilisha kanuni hizo kutokana na mapendekezo ya wademokrats walio wachache katika baraza hilo.
Wademokrats walitaka hati muhimu kuhusiana na kesi hiyo kutolewa na utawala wa Trump pamoja na kuruhusu mashahidi kusikilizwa ambao ni washauri wa karibu wa rais wa sasa na wa zamani.
Wakili Mkuu wa Trump Pat Cipollone ameeleza kanuni hizo zilizo wasilishwa na Mkuu wa Baraza la Senate kuwa ni njia sawa ambayo itapelekea kwa rais kutopatikana na hatia.
Naye Mbunge Adam Schiff anaye ongoza tume ya wabunge kama waendesha mashtaka anasema kutoruhusu mashahidi na hati kuwasilishwa mbele ya baraza hilo kutaifanya kesi hiyo kuwa jambo la dhihaka.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.