Vipi hatua ya Xi kuwaondoa viongozi waandamizi wa makampuni ya anga na Ulinzi itaidhoofisha kijeshi China

Rais wa China Xi Jinping

Viongozi watatu katika nafasi muhimu kwenye  makampuni ya anga za juu na ulinzi wameondolewa kwenye nyadhifa za juu za kisiasa katika kitengo cha  ushauri cha Chama cha Kikomunisti.

Wakati huo huo Beijing inaendeleza juhudi zake za kuwaondoa viongozi wa juu katika jeshi la China, shirika la habari rasmi la Xinhua lilisema Alhamisi.

Hatua ya kulisafisha jeshi ni sehemu ya kampeni ya kihistoria ya kiongozi wa China Xi Jinping ambayo itapelekea makamanda kadhaa wa ngazi ya juu kuondolewa katika nafasi zao na kukabiliwa na uchunguzi unaohusiana na rushwa.

Kampeni dhidi ya ufisadi inaonekana na baadhi ya wataalam kama njia ya Xi kuwaondoa wapinzani wake wa kisiasa au watu binafsi ambao wanaonekana kuwa ni tishio kwa uongozi wake.

Xinhua limesema kuwa Baraza la Ushauri wa Kisiasa la Watu wa China liliamua Jumatano kuwafukuza kazi Wu Yansheng, mwenyekiti wa Shirika la China Aerospace Science and Technology, Liu Shiquan, mwenyekiti wa Norinco Group, na Wang Changqing, naibu meneja wa shirika linalomilikiwa na serikali la China Aerospace Science and Industry.

Moja ya uzinduzi wa chombo cha anga za juu unaofanywa na shirika la China Aerospace Science and Technology Corporation)

Kampuni ya Wu inasimamia uendelezaji wa program za anga za juu na makombora za China, na kampuni anayoisimamia Liu ya Norinco Group ni moja ya kampuni zinazoongoza za China katika utengenezaji wa vifaa vya kijeshi.

Vyombo vya habari vya serikali havikutoa maelezo zaidi kuhusu kuondolewa kwa watu hao, lakini ripoti moja ya gazeti litolewalo kila siku la Sing Tao Daily la Hong Kong lilidai kuwa watatu hao walihusishwa na uchunguzi unaohusiana na kikosi cha roketi cha jeshi la China, likinukuu vyanzo vilivyokuwa havikutajwa.

Baadhi ya wachambuzi wanasema wimbi la karibuni la kuwaondoa viongozi linaonyesha kiwango kikubwa cha ufisadi katika sekta ya ulinzi ya China na kuwa inaweza kuathiri uwezo wa jeshi la China kivita.

“Nafikiri inawezekana kuna kiwango kikubwa cha ufisadi katika sekta ya ulinzi ya China na hilo halizuiliki, litakuwa na athari mbaya kwa uwezo wa kivita wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa China,” Lin Ying-yu, mtaalam wa kijeshi wa China aliyeko katika Chuo Kikuu cha Tamkang huko Taiwan, aliiambia VOA kwa simu.

Alisema zoezi hili la kuwaondoa viongozi katika jeshi linaonyesha pia azma ya Xi kuongeza udhibiti wa biashara ya silaha nchini China.

“Katika siku za nyuma, sehemu kubwa ya biashara ya silaha za China ilikuwa inadhibitiwa na princelings, ambao ni warithi wa viongozi wa ngazi ya juu ya Chama cha Kikomunisti,” aliiambia VOA.

“Huenda ikawa kuondolewa huku kwa viongozi kuna maanisha Xi anataka kuweka wazi udhibiti wake wa biashara ya silaha.”

Mbali na kuathiri uwezo wa jeshi la China na kumpa nguvu Xi kudhibiti biashara ya silaha, wataalam wengine wanasema hatua hiyo ya ghafla ya kuwaondoa makamanda wa juu wa jeshi inaweza kuvunja morali katika jeshi la China na kutokea changamoto kadhaa katika Xi kulidhibiti jeshi.

“Mlolongo huu wa kashfa za ufisadi unaweza kutengeneza mashaka ndani ya jeshi juu ya uaminifu wa uongozi wa juu na kutengeneza mzunguko wa uasi ambao hatimaye utaathiri uwezo wa Xi kudhibiti,” Su Tzu- yun, mtaalam wa kijeshi katika taasisi ya utafiti ya National Defense and Security yenye makao yake Taipei, ameiambia VOA kwa simu.

Ripoti ya Mwandishi wa VOA William Yang