Tanzania : Waziri Mhagama, Mkuu wa SSRA watakiwa kuwajibika

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, SSRA, Irene Isaka

Mtalaam wa sayansi ya siasa na utawala wa umma nchini Tanzania, Profesa Mwesiga Baregu, amesema kwa hatua iliyochukuliwa na Rais John Magufuli ya kubatilisha mfumo mpya wa upigaji mahesabu (Kikokotoo) ya mafao ya wastaafu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Jenister Mhagama analazimika kujiuzulu.

Vyanzo vya habari vimeripoti Jumamosi Profesa Baregu amemtaka pia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, SSRA, Irene Isaka, kuachia ngazi kwa kuwa wawili hao wametoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki kwa umma.

Rais atoa tamko

Wakati huohuo Rais Magufuli amesema upigaji mahesabu ya mafao ya wastaafu wa sekta binafsi na serikalini yataendelea kufuata mfumo wa zamani wa asilimia 25 kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na asilimia 50 kwa wafanyakazi wa serikali hadi 2023.

Sheria ya hifadhi ya jamii

Januari, 2018, Bunge lilipitisha sheria ya hifadhi ya jamii, ambayo pamoja na mambo mengine iliunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka sita na kuwa miwili. Mifuko iliyokuwa awali ni Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Mfuko wa Pensheni wa PPF, Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) na NSSF.

Mifuko miwili hiyo mipya ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta Binafsi na Isiyo Rasmi (NSSF) na ule wa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF).

Hatimaye sheria hiyo ilitiwa saini na Rais John Magufuli kwa ajili ya kuanza kutumika lakini kabla ya kutumika rasmi, ilipaswa kutungiwa kanuni ambazo pamoja na mambo mengine, zingeainisha kikokotoo cha mafao.

Nasaha kwa serikali

"Katika hali ya kawaida kwenye mfumo wa demokrasia, demokrasia inayofanya kazi na yenye uhai, nilitegemea (viongozi hao) wajiuzulu kwa sababu wamempotosha Rais kwa ushauri wao na Rais mwenyewe analalamika, amesema Profesa Baregu.

“Ujumbe ni kwamba mtu unapokwenda kinyume cha maadili katika wajibu wako, unatakiwa ukae kando kwa kushindwa kutekeza wajibu wao kwa kuacha kutoa ushauri makini kwa Rais,” alisema.

Shinikizo la Chadema

Mbali na Baregu, Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) ambaye pia ni waziri Kivuli mwenye dhamana ya Kazi na Ajira, Ester Bulaya pia aliwataka Mhagama na Isaka waachie ngazi.

“Sasa Mheshimiwa Jenista (Mhagama) na Mkurugenzi wa SSRA, mjiuzulu nimewashinda…hamkuwatetea wafanyakazi,” alisema Bulaya katika ujumbe wake aliouandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Hoja ya Bulaya juu ya kikokotoo

Bulaya ndiye aliyeibua hoja juu ya kikokotoo hicho hatua ambayo ilisababisha Isaka kumjinu tena kwa kejeli na vijembe.

Baada ya hapo, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) kwa kushirikiana na SSRA iliandaa semina kwa ajili ya wahariri wa vyombo vya habari mjini Dodoma kuelezea umuhimu wa kanuni hiyo, huku ikieleza kinagaubaga kwamba ni mkombozi kwa wafanyakazi.

Baadaye, SSRA ilitoa ufafanuzi juu ya utaratibu huo mpya wa mahesabu ya mafao ya wastaafu kwamba mstaafu atapata mafao ya 1/580 kwa mkupuo kisha kuendelea kulipwa kila mwezi kwa muda wa miaka 12.5 na iwapo angefariki dunia kabla ya muda huo, mafao yake yatatumika kusomesha watoto wake.

Mchango wa Ester Bulaya

Baada ya SSRA kutoa ufafanuzi huo uliotokana na baadhi ya vyombo vya habari, ulianza upinzani kutoka kila upande huku Waziri Kivuli mwenye dhamana ya Kazi na Ajira, Ester Bulaya, akaibuka na kusema bunge lilidanganywa kuhusu jambo hilo.

Bulaya, ambaye ni Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), alisema wabunge walitaka mfumo wa upigaji mahesabu ya mafao ya wafanyakazi (Kikokotooo) uainishwe kwenye sheria lakini serikali ilisema itakiweka kwenye kanuni na matokeo yake ilitunga kitu alisema ambacho kinawakandamiza wastaafu.

Hoja binafsi

Mbunge huyo ambaye awali alikuwa CCM kabla ya kujiunga na upinzani, alisema kutokana na kanuni hiyo kuwa kandamizi na mzigo kwa mfanyakazi, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni.

Wakati Bulaya akiweka bayana jambo hilo, wadau mbalimbali waliibuka na kulishambulia bunge kuwa limetunga sheria ambayo inawaumiza wananchi huku wakishangaa wabunge kutowajali wananchi wakati wao wanachukua mafao yao yote bila kukatwa chochote.

Jambo hilo lilimwibua Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alikanusha hilo na kusema bunge linabebeshwa mzigo wa lawama lisiostahili kwa kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitungi kanuni bali sheria.

Ndugai alisisitiza kuwa kama kuna mtu yeyote anaona kanuni hiyo ni kandamizi anapaswa kuiwasilisha Bungeni kupitia Kamati ya Sheria Ndogo iliyo chini ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ili hatua zaidi zichukuliwe ikiwamo kuiagiza serikali kuifanyia marekebisho.

TUCTA yaja juu

Hatimaye Tucta iliibuka na kupinga kanuni hiyo kuwa itasababisha maumivu makali kwa wastaafu huku ikisisitiza kuwa miongoni mwao wanaweza kukumbwa na maradhi ikiwamo msongo wa mawazo na hata kupoteza maisha.

Tucta pia ilisema hata wakati wa majadiliano juu ya kanuni hiyo kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya serikali na waajiri kwa upande mmoja na Tucta upande mwingine, hatua iliyosababisha hata wakati wa upigaji kura upande wa serikali na waajiri ulishinda.

Kutokana na kanuni hiyo kuwa kandamizi, Tucta iliiomba serikali kurejea kwenye meza ya mazungumzo na wadau, wakiwamo wafanyakazi kupitia vyama vyao ili kuifanyia marekebisho kanuni hiyo.

Shinikizo la vyama vya wafanyakazi

Vyama takriban vyote vya wafanyakazi, vikiwamo Chama cha Walimu (CWT), Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu), Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (THTU), vilipinga kanuni hiyo huku vikisisitiza serikali kukaa meza moja na wadau ili kuleta mtangamano juu ya jambo