Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana hofu ya kurudi kwa kundi la Taliban madarakani nchini Afghanistan.
Guterres ameeleza kuwa huenda kurudi huko kwa Taliban kukayapatia makundi ya wanamgambo wa Kiislamu huko Kanda ya Sahel ya Afrika Magharibi motisha wa kujiimarisha.
Katika mahojiano yake hapo Alhamisi Guterres ametoa wito wa kuimarishwa mfumo wa usalama kwenye kanda hiyo.
Anasema kuna hatari kubwa kwa makundi haya ya kigaidi kuhisi kwamba yanaweza kupata nguvu kutokana na kilichotokea Afghanistan na kuwa na matarajio makubwa zaidi kuliko walivyo kua nayo miezi michache iliyopita.
Guterres amesema ni muhimu kuimarisha mfumo wa usalama ingawa Ufaransa na Chad zimetangaza azma ya kuondoa wanajeshi wake kutoka kanda hiyo.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la Habari la AFP