Uhamiaji, Iran na huduma ya afya vyagubika mdahalo wa Wademokrat

Wagombea urais wa chama cha Demokrat, kutoka kushoto, Cory Booker, Elizabeth Warren, Julian Castro, Bill de Blasio, Tulsi Gabbard, Amy Klobuchar, Jay Inslee, na muogozaji mdahalo Chuck Todd, Beto O’Rourke na John Delaney wakisalimiana baada ya kumaliza mdahalo.

Kundi la kwanza la wagombea Urais 10 kupitia chama cha Democratic nchini Marekani, 2020, wamefanya mdahalo wao wa kwanza Jumatano, Miami, Florida, kwa masaa mawili ambao umezingatia masuala ya huduma za afya, mustakbali wa mazungumzo na Iran na mabadiliko ya hali ya hewa.

Uhamiaji

Katika yale ambayo yalijadiliwa katika mdahalo huo ni pamoja na huduma ya afya, sera za kigeni, ukatili unaotokana na umiliki wa silaha, na uhamiaji. Suala la uhamiaji lilifunikwa na taarifa mpya za kutisha juu ya hali ya vituo vinavyowazuia wakimbizi vilivyofurika wahamiaji wasiokuwa na makaratasi katika mpaka wa kusini mwa Marekani.

Huduma ya Afya

Seneta wa zamani wa Texas Beto O’Rourke amezungumzia jinsi atakavyo lishughulikia suala hilo kwa njia tofauti na ile yenye utata ambayo Trump amechukuwa ya sera ya “kutokuwa na simile.”

Kwa upande wake Seneta wa Marekani Elizabeth Warren, ambaye ni miongoni mwa wagombea wanaoongoza katika kinyang'anyiro hicho amesema atapigania huduma ya afya inayofadhiliwa na serikali na kuwakosoa wale ambao wanapinga mfumo wa afya wa aina hiyo.

"Wanao waeleza kwamba hawataki kulipigania hilo," amesema Warren. "Huduma ya afya ni huduma ya msingi kwa binadamu na mimi nitapigania haki za msingi za binadamu. "

Katika ajenda ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 suala la afya limekuwa ni kipaombele, hasa baada ya Rais Donald Trump kutumia amri ya kiutendaji kufuta sehemu ya mpango wa afya wa rais aliyemtangulia Barack Obama, maarufu kwa jina la Obamacare.

Mustakbali wa Iran

Kuhusu suala la Iran, Seneta wa jimbo la New Jersey Corey Booker alikuwa mgombea pekee kusema kuwa haungi mkono makubaliano ya nyuklia na Iran na kuiita "uamuzi wenye makosa."

Hadi sasa mkataba wa nyuklia wa Iran umekuwa mjadala mkubwa miongoni mwa wapiga kura wa Marekani, wakati nchi hiyo ikiwa na mvutano na Marekani kuhusu mashambulizi ya meli za kubebea mafuta yaliyotokea Ghuba ya Uajemi hivi karibuni. Hata hivyo baadhi ya wagombea waliyapa masuala mengine ya usalama kipaumbele zaidi.

Mabadiliko ya Tabia Nchi

Katika hoja yake wakati wa mdahalo huo wa kundi la kwanza Gavana wa jimbo la Washington Jay Inslee amesema amestaajabishwa kuona kuwa suala la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi halikupewa kipaumbele na wagombea wengi katika mdahalo huo.

Inslee kwa masikitiko makubwa amesema kizazi cha leo ndiyo cha kwanza kushuhudia uchungu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na ndiyo cha mwisho kinachojaribu kupambana na hali hiyo.

Makamu wa rais wa zamani Joe Biden na Seneta Bernie Sanders, wanaoongoza katika kura za maoni watapambana katika sehemu ya pili ya mdahalo huo Alhamisi jioni.