Trump na mawakili wake wakuu wahitalafiana kabla ya kesi

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump akionyesha gazeti la USA Today likiwa na habari za Baraza la Seneti kumuondolea mashtaka kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka na kuingilia kati Bunge la Marekani, Washington, Marekani, February 6, 2020. REUTERS/Leah Millis

Ikiwa imebakia chini ya wiki moja kabla ya kuanza kesi yake ya pili iliyofunguliwa katika Baraza la Seneti, timu ya mawakili wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump inaelekea kuhitalafiana.

Mawakili wawili mashuhuri kutoka jimbo la South Carolina, Butch Bowers na Deborah Barbier, walitarajiwa kuwa ni mawakili viongozi wa Trump. Lakini, taarifa za vyombo vya habari Jumamosi zimesema kumekuwa na makubaliano ya kutomwakilisha Trump katika kesi hiyo.

Zaidi ya hilo, mawakili wengine watatu walioripotiwa kufanya kazi na rais pia hawatakuwepo tena katika timu ya mawakili wa Trump, kwa mujibu wa taarifa zilizo tolewa awali na CNN.

Trump na mawakili hao wanaripotiwa kutokubaliana juu ya mkakati upi wa kisheria utafaa kukabiliana na kesi iliyopangwa kusikilizwa Februari 9.

Rais wa zamani Donald Trump

Rais wa zamani anakabiliwa na mashtaka ya “uchochezi wa uasi” unaohusiana na genge lililovamia Bunge la Marekani Januari 6. Amepangiwa kujibu mashtaka hayo siku ya Jumanne.

Vyanzo vya habari vinasema Trump anataka mawakili wake kuangaza dhana ya uongo kuwa alishindwa uchaguzi wa urais dhidi ya Joe Biden kwa sababu ya kuwa muathirika wa wizi wa kura uliosambaa, badala ya kutizama tuhuma dhidi yake za uasi.

FILE - Genge la Rais wa zamani Donald Trump likiwashambulia maafisa wa polisi wa Bunge la Marekani walipovamia bungeni, mjini Washington Jan. 6, 2021.

Wachambuzi wanasema rais wa zamani huyo kuna uwezekano mkubwa wa kutokutwa na hatia kufuatia hatua ya maseneta Warepublikan 45 waliopiga kura hivi karibuni kuwa kesi hiyo ni kinyume cha katiba kwa sababu Trump hayuko tena madarakani.

Trump ni rais wa kwanza wa Marekani kushtakiwa kuondolewa madarakani. Mwaka mmoja uliopita Baraza la Seneti lilimuondolea mashtaka kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka na kuingilia kati Bunge la Marekani.