Kwenye ujumbe wa Twitter, Trump ameandika kwamba Joseph Maguire, ambaye amekuwa ni Mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha kupambana na ugaidi, atakuwa kaimu mkurugenzi wa Idara Kuu ya Ujasusi wa kitaifa kuanzia Agosti 15, siku Coats na Gordon wanaondoka ofisini.
Trump hajatangaza chaguo lake la mtu atakayehudumu kama mkurugenzi mkuuwa shirika la kitaifa la ujasusi.
Rais Donald Trump katika ujumbe mwengine wa Twitter alisema amekubali hatua ya kujiuzulu kwa naibu wa mkurugenzi mkuu wa idara hiyo ya ujasusi ya kitaifa Sue Gordon, Alhamisi jioni.
Gordon anajiuzulu siku chache baada ya kusema alikuwa na nia ya kuwa kaimu mkurugenzi wa shirika hilo.
Barua ya Gordon ya kujiuzulu, aliyomuandikia Trump, inasemekana inaeleza wazi kwamba haondoki ofisini kwa kupenda kwake.
Amemuambia Trump kwamba barua yake ni hatua ya heshima na uzalendo, wala sio kupenda kwake, na kwamba Trump anastahili kuwa na timu yake.
Kuondoka kwa Gordon kutoka shirika la ujasusi, ni hatua inayojiri wiki mbili baada ya mkurugenzi wa idara ya ujasusi, Dan Coats, kutangaza kwamba anaacha kazi mwezi ujao, Agosti 15.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.