Rais wa Russia, Vladimir Putin alikusudia kuvuruga uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016 na kumchafua aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekan, Hillary Clinton katika “kampeni chafu” ambayo haijawahi kutokea.
Hatimaye rais huyo aliamua kumsaidia rais mteule, Donald Trump, imesema taarifa ya ripoti iliyoidhinishwa kutumika kwa umma na jumuiya ya vyombo vya upelelezi vya Marekani.
Dhamiri ya Russia ilikuwa kufanya umma upoteze imani katika mchakato wa demokrasia ya Marekani, kumdhalilisha waziri Clinton, na kuchafua nafasi yake ya kuchaguliwa,” kwa mujibu wa hiyo taarifa iliyotolewa baadae Ijumaa.
“Pia tuliweza kugundua Putin na serikali ya Russia walitengeneza mkakati wa upendeleo kwa rais mteule Trump,” ripoti iliendelea kueleza ikiongeza kuwa Putin na serikali ya Russia walikusudia kumsaidia kutengeneza mazingira makubwa ya kuchaguliwa rais mteule Trump kadiri walivyoweza.”
Kutolewa kwa ripoti hiyo na mashirika matatu ya kipelelezi ya Marekani kumekuja baada ya saa chache kwa viongozi wa mashirika hayo kumpa muhtasari wa taarifa za kipelelezi za siri Trump huko New York.
Rais anayemaliza muda wake, Barack Obama ambaye aliamuru kuandaliwa kwa ripoti hiyo, yeye alipewa muhtasari huo wa kipelelezi siku ya Alhamisi.
Katika ripoti hiyo taasisi zote mbili CIA na FBI wanaeleza kuwa wana imani kubwa na majumuisho ya taarifa hizo.
Idara ya usalama wa taifa (NSA), wakati wakionyesha kukubaliana na taarifa hiyo walisema kwa kiasi fulani ina imani na majumuisho hayo.
Ijumaa jioni, Trump alituma ujumbe wa twitter akikilaumu chama cha Demokratik kwa kutokuwa makini na kuweza kuingiliwa na wahalifu wa mitandao.
“Huo ni uzembe wa kamati ya Demokratiki ambayo iliruhusu mchezo mchafu wa mitandao ufanyike,” alisema Trump katika Tweet.
“Bila ya shaka kamati ya Republikan ilikuwa makini na ulinzi mkali.”
Trump aliendelea kukilaumu chama cha Demokratik katika Twitter zake Jumamosi asubuhi, akidai kuwa uhalifu wa mitandao haukubadilisha upigaji kura na kudai kuwa wademokrat “wamepigwa na butwaa” kwa kupoteza uchaguzi.
“Taarifa za kipelelezi zimeeleza kwa ufasaha hakuna ushahidi kwamba uhalifu wa mitandao umeathiri matokeo ya uchaguzi,” Trump alituma ujumbe huu kwenye Twitter.
“Sababu pekee leo uhalifu wa mitandao ulioathiri kamati ya Demokratik unazungumziwa ni kwa sababu kushindwa kwa chama hicho ilikuwa pigo kubwa na bado wamebutwaa!”