Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 23:23

Trump azuru CIA: ‘Niko pamoja na nyinyi’


Trump akizungumza na wafanyakazi wa CIA
Trump akizungumza na wafanyakazi wa CIA

Trump ametoa matamshi hayo kwenye makao makuu ya idara hiyo huko Langley, Virginia Jumamosi, katika siku ya kwanza akiwa rais wa Marekani.

“Najua kwamba wakati mwengine pengine hamjapata msaada mliokuwa mnautaka na sasa mtapata msaada mwingi zaidi. Labda mnaweza kusema, ‘tafadhali usitupe msaada mwingi zaidi,’ amesema kiongozi huyu mpya aliyeapishwa, na kusababisha kicheko.

Maafisa wa CIA wamesema kuwa takriban wafanyakazi 400 wa CIA walihudhuria wakati rais anatoa kauli yake.

Vita dhidi ya Islamic State

Trump ameweka wazi kuwa vita dhidi ya kundi la Islamic State itakuwa ndio kipaumbele na uongozi wake utakazia mwelekeo wa Marekani katika mapambano haya.

“Tumekuwa tukipigana vita hivi kwa muda mrefu kuliko vita vyovyote tulivyowahi kupigana,” amesema. Hatujatumia nguvu zetu halisi tulizokuwa nazo, tumekuwa tukibanwa. Ni lazima tuimalize kabisa ISIS, tuiangamize kabisa ISIS. Hatuna namna.

Juhudi za Kurejesha masikilizano

Ziara ya rais ni juhudi ya kurejesha masikilizano na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa upelelezi, kwa mujibu wa wachambuzi.

Ni aina fulani ya kuonyesha maelewano kwa jumuiya ya upelelezi,” amesema Aki Peritz, mchambuzi wa zamani wa masuala ya kupambana na ugaidi na mwandishi mwenza wa kitabu kinachoelezea namna ya kutokomeza ugaidi, kinachoitwa: Find, Fix, Finish: Inside the Counterterrorism Campaigns that Killed bin Laden and Devastated Al Qaeda.

Maafisa wa upelelezi wamekuwa wakidadisi kauli za dharau za Trump kuhusu idara hizi za kijasusi na kazi zao imewavunja moyo wafanyakazi.

“Wafanyakazi wa CIA wote ni mahiri sana, ni wenye weledi wa kazi zao, na wameelimika vizuri,” alisema Peritz. “Hotuba moja haiwezi kuondoa manung’uniko yao makubwa waliyokuwa nayo juu ya rais huyu wa sasa.

Kwa miezi kadhaa, Trump amekataa kukubaliana na muhtasari wa uchunguzi uliotolewa na CIA na idara ya Upelelezi FBI kuwa Russia lilifanya udukuzi kwenye mkutano wa chama cha Demokratik wenye lengo la kuvuruga uchaguzi wa Marekani, na kwa namna fulani ulikuwa unamsaidia Trump ashinde uchaguzi.

Lakini ilichukuwa muda hadi hapo Januari 11 katika mkutano wa waandishi wa habari ndipo Trump alipokiri “Nafikiri ilikuwa Russia” waliofanya kitendo hicho cha udukuzi, lakini baadae akaongeza inawezekana ikawa mtu mwengine, ikiwemo China.

Rais mpya wa Marekani ameendelea kukanusha madai ya Moscow kuhusika na udukuzi huu uliomkandamiza hasimu wake wa Chama cha Demokratik Hillary Clinton na kumsaidia yeye kuingia ikulu ya White House.

Pia amerejea mara nyingi kutaja makosa ya vyombo hivyo vya kipelelezi yaliyotokea siku za nyuma na kudai kuwa jumuiya ya kipelelezi inawezekana ilihusika na kuvujisha taarifa zilizokuwa hazijathibitishwa kuwa Russia ina taarifa ambazo zinaweza kuwapa fursa ya kumdhibiti.

Wakati akitoa maoni yake Jumamosi, Trump amesema sababu ya kufanya ziara ni kutokana na sintofaham inayoendelea kati yake na vyombo vya habari,” na kuelezea kuwa vyombo vya habari “vimefanya ionekane kama mimi nina vita na jumuiya ya kipelelezi.”

Asema CIA kupata chapakazi

Ziara ya Trump CIA imefuatia baada ya wabunge wa Demokratik walipofanikiwa kuzuia mpaka Jumatatu maamuzi ya baraza la Seneti juu ya chaguo la Trump, katika nafasi ya mtendaji wa CIA, Mike Pompeo, mrepublikan akishutumu kuwa kucheleweshwa kupitishwa kumeifanya idara hiyo ya kijasusi kutokuwa na uongozi muda wote wamwishoni mwa wiki.

Trump amemsifia Pompeo, na kuwaambia wafanyakazi wa CIA chaguo lake ni muafaka kwa kazi hiyo.

“Mtampata nyota kamili . Hakika mnaletewa mchapakazi,” alisema.

Afisa mwengine wa zamani wa CIA amehoji sababu iliyomfanya rais kuzuru idara hiyo siku ya wikiendi. Kwa kawaida, ziara hizi hufanyika siku za kazi wakati wafanyakazi wengi wanakuwepo kazini. Mara nyingi, kunakuwa na kupanga mstari ambapo anapata fursa ya kusalimiana nao.

“Kuna juhudi zilizofanyika kufanya ziara hiyokurejesha morali za wafanyakazi,” amesema Carmen Medina, Naibu Mkurugenzi wa zamani wa CIA.

“Inaonyesha kuna mambo yanayoweza kuhusiana namna fulani na masuala ya usalama wa taifa na mambo ya kipelelezi, ambapo inawezekana rais ameomba kupewa muhtasari au jumuiya ya kipelelezi imependekeza apokee muhtasari huo,” mwanamke huyo amesema.

Kabla ya kutembelea makao makuu ya CIA, rais mpya aliyeapishwa—pamoja na familia yake na makamu rais, Mike Pence na mkewe, Karen—walihudhuria ibada maalum katika kanisa la taifa la Cathedral Washington.

Rais Donald Trump na Makamu wake Mike Pence na familia zao wahudhuria ibada maalum
Rais Donald Trump na Makamu wake Mike Pence na familia zao wahudhuria ibada maalum

Mapema Jumamosi, Trump alituma ujumbe wa Twitter kuelezea shukrani zake kwa wamarekani kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake Ijumaa na kuvishukuru vyombo vya habari kwa maoni yao na tahariri zao nzuri kuhusu kuapishwa kwake.

XS
SM
MD
LG