Somalia : Mlipuko wa bomu Mogadishu wauwa 76, wakiwemo wanafunzi

Mlipuko wa bomu uliotokea katika eneo la kukagua magari mjini Mogadishu, Somalia, Disemba 28, 2019. REUTERS/Feisal Omar - RC284E9MPBR5

Mlipuko wa bomu mjini Mogadishu, Somalia umeuwa watu zaidi ya 76, ofisi ya huduma ya dharura kwa wagonjwa imeeleza Jumamosi.

Meya wa Mogadishu Omar Mohamud Mohamed (Omar Filish) amesema Jumamosi wengi kati ya wahanga wa mlipuko huo ni raia wakiwemo wanafunzi wengi waliokuwa wanaelekea shuleni na vyuoni. Amesema wengine walikuwa wamejeruhiwa.

Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari lililipuka wakati harakati katika eneo la makao makuu ya nchi hiyo, Mogadishu zikiwa zimeshika kasi.

Afisa wa Polisi Ibrahim Mohamed amethibitisha kutokea mlipuko huo na vifo, limeripoti shirika la habari la AFP.

Mlipuko huo ulitokea katika kituo kimojawapo cha kukagua magari eneo la makutano ya njia panda mjini Mogadishu.

Ubalozi wa Uturuki umeiambia VOA kuwa raia wake wawili waliokuwa wanafanya kazi katika kampuni ya ujenzi walikuwa kati ya waliouawa na bomu hilo.