Shambulizi Australia lauwa mmoja, mwengine mahtuti

Afisa polisi wa Victoria akifanya uchunguzi katika eneo la tukio la uhalifu ambapo risasi kadhaa zilitumika katika shambulizi hilo katika klabu ya Love Machine, Prahran, Melbourne, Australia, Aprili 14, 2019.

Shambulizi la bunduki lililofanywa na mtu aliyekuwa ndani ya gari lililokuwa katika mwendo, nje ya nyumba ya starehe ambayo ni maarufu mjini Melbourne, Australia mapema Jumapili, lilisababisha mtu mmoja kuuawa na mwengine kujeruhiwa vibaya na wengine wawili kupata majeraha, polisi wameeleza.

Polisi wamesema kuwa bunduki ilipigwa kutoka katika gari ikilenga umati wa watu waliokuwa wamesimama nje ya klabu hiyo ya starehe ya ghorofa mbili ijulikanayo kama klabu ya Love Machine, na kuwaathiri walinzi watatu katika sehemu hiyo ya starehe na msimamizi mmoja wa klabu hiyo.

Polisi wametangaza kuwa mtu yeyote aliyekuwa na picha za video au taarifa kuhusu tukio hilo kujitokeza. Mpaka sasa hawajamkamata mtu yeyote kuhusiana na tukio hili.

Watu wanne waliojeruhiwa walipelekwa hospitali, wawili kati yao wakiwa mahututi. Polisi baadae walithibitisha kuwa mwanaume mmoja, 37, alipoteza maisha.

Wanaendelea na uchunguzi ili kujua iwapo gari aina ya Porsche SUV nyeusi iliyokuwa ikiondoka katika eneo hilo inahusika katika shambulizi hilo la bunduki. Gari hilo baadae lilipatikana likiwa limechomwa moto.

“Mambo haya yakustaajabisha bado ni nadra kutokea, na hakuna tetesi yeyote inayoonyesha hivi sasa kuwa tukio hili ni sehemu ya ajenda pana zaidi ya uhalifu,” amesema Andrew Stamper wa jeshi la polisi la jimbo la Victoria.

Baada ya tukio hilo Afisa polisi wa Victoria alifika kufanya uchunguzi katika eneo lililotokea shambulizi la kutumia bunduki ambapo risasi kadhaa zilitumika nje ya klabu ya Love Machine iliyoko Prahran, mjini Melbourne, Australia, Aprili 14, 2019.

Mmiliki wa Love Machine, Steve Yousif alichapisha katika mtandao wa Facebook : “Tumeelemewa na simu mlizotupigia na ujumbe wa simu mliotutumia, hakuna zaidi ila ni upendo wetu kwenu nyote.”

“Kilichotokea jana usiku ni jambo halikustahili na limetushitua. Kwa baadhi yenu ilikuwa ni usiku wa starehe, kwa familia yote ya klabu ya Love Machine imepoteza mtu mwenye roho nzuri hivi leo,” aliandika mmiliki huyo.

Uhalifu wa silaha ni nadra nchini Australia, ambayo iliboresha sheria za udhibiti wa silaha kufuatia shambulizi lililofanywa na mtu mmoja mwenye bunduki mwaka 1996 huko katika mji wa Tasmania mwaka 1996, na kuuwa watu 35.

Huko nchini New Zealand, mzungu mmoja raia wa Australia mbaguzi amefunguliwa mashtaka ya mauaji ya mashambulizi aliyoyafanya katika msikiti na kuuwa watu 50, iliyopelekea nchi hiyo kupiga marufuku umiliki aina kadhaa ya silaha za kivita.