Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:46

Miili ya waliouawa New Zealand yatolewa kwa familia


New Zealand Mosque Shootings
New Zealand Mosque Shootings

Mamlaka nchini New Zealand, zimeanza kupeana baadhi ya miili ya watu waliouwawa Ijumaa iliyopita katika tukio la kufyatuliwa risasi kwenye misikiti miwili na mwanaume ambaye ametajwa kuwa mbaguzi.

Polisi wanasema uchunguzi wa miili hiyo umekamilika lakini ni maiti 12 tu ndio wametambuliwa rasmi, na kwamba katika kundi hilo, sita wamepeanwa kwa wana familia.

Taarifa iliyotolewa na polisi wa mji wa Christchurch imesema kwamba wakati utambuaji wa maiti ukionekana kuwa ni rahisi, ukweli ni kwamba umekuwa mgumu hasa katika hali kama hiyo.

Majina ya waliouwawa bado hayajatangazwa kwa umma ijapokuwa orodha ya awali imetolewa kwa familia.

Waziri mkuu Jacinda Ardern amesema kwamba kufikia Jumatano wiki hii, miili yote itakuwa imerudishiwa familia husika.

Siku ya Jumamosi mtu anayeshukiwa kuwa na itikadi za mrengo wa kulia, Brenton Tarrant, alifikishwa mahakamani nchini New Zealand kufuatia mashambulizi hayo, yaliyofanyika mjini Christchurch.

Tarrant, mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni raia wa Australia, akiwa amefungwa pingu alisimama kimya mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Christchurch kabla ya kurudihwa rumande bila ya kusema chochote.

Kulingana na vyombo vya usalama, watu 34 bado wamelazwa hospitalini.

XS
SM
MD
LG