Saudi Arabia yawashikilia wakosoaji wa mauaji ya Jamal Khashoggi

Marehemu Jamal Khashoggi

Saudi Arabia imewakamata watu wanane wakiwemo raia wawili wa Marekani wenye asili ya Saudi Arabia. Shirika la habari la Associated press linaripoti kwamba waliokamatwa ni pamoja na mwanamke mmoja mjamzito na wanaume saba.

Watu wote waliokamatwa wanaishi Saudi Arabia na wamekuwa wakiunga mkono haki za wanawake na kukosoa mauaji ya Jamal Khashoggi.

Kukamatwa kwa watu hao ni zoezi la kwanza la kuwafuatilia wakosowaji wa taifa hilo la kifalme tangu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyeuwawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Instanbul mwezi Oktoba mwaka 2018.

Kundi la kutetea haki za binadamu lenye makao yake Uingereza, ALQST, linaeleza watu wote waliokamatwa walikuwa waandishi na ma-blogi za mitandao ya kijamii ambao awali walijihusisha katika mijadala ya hadhara juu ya mageuzi.

Watu wengi waliokamatwa jana Alhamis. Badr al-Ibrahim, ambaye ni mwandishi na pia daktari, ni mmoja wa raia wawili wa Kimarekani wenye asili ya Saudi Arabia, waliokamatwa.

Salah al-Haidar ni raia mwingine wa Marekani, mtoto wa mwanaharakati Aziza al-Yousef, ambaye tayari yupo gerezani na wanawake 10 wengine kwa takribani mwaka mmoja na kumekuwepo na shutuma za kuteswa na unyanyasaji wa ngono.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.