Hali hiyo inaweza kutatuliwa tu iwapo wamiliki wa usafiri wa abiria watakaa chini na kutafuta suluhu ya kudumu, Gideon Moi amesema.
Seneta wa Baringo, Moi ametaka ofisi ya meya kuchukuwa hatua za haraka kutatua tatizo hilo la usafiri akisisitiza kuwa utekelezaji mbovu wa agizo la kuzuia matatu kuingia mjini halikuwa na manufaa.
Amewataka wadau wa vyombo vya usafiri na wataalam wa usafirishaji kutafuta suluhu ya maridhiano katika mgogoro huu wa usafiri jijini Nairobi mara moja.
“Leo tumeshuhudia abiria wakiwa mashakani baada ya kulazimika kutembea kwa masafa marefu kwenda makazini, na katika biashara zao ndogo ndogo wakilazimika kulipa gharama zaidi za kusafirisha bidhaa zao kufikia soko, ikileta usumbufu katika biashara zao na watu wazima wakiwa wamekwama katika maeneo mabasi yalipo washusha wakiwa hawana usafiri mbadala wala mtu yeyote wakuwasaidia,” amesema.
Moi hivi sasa anataka ofisi ya Meya kuanzisha usafiri wa bei nafuu na wenye kufuata mpangilio bora kwa ajili ya kuwahudumia wasafiri kutoka katika vituo vilivyokuwa vimeandaliwa washuke na kuchukuliwa kwenda ndani ya eneo la biashara la jiji la Nairobi.