Sababu za Marekani kutoishambulia Iran kama ilivyopanga hazijulikani

Rais Donald Trump

Maafisa wa usalama wa taifa mjini Washington, wamekataa kuzungumzia ripoti za vyombo vya habari kwamba Rais Donald Trump aliidhinisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, Alhamisi, lakini wakasitisha mpango wa kuanza mashambulizi hayo kutokana na sababu zisizojulikana.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, Trump aliamrisha mashambulizi dhidi ya sehemu maalum za Iran kama mitambo ya kuchunguza safari za ndege, na mitambo ya kurusha makombora.

Gazeti la Washington Post na vyombo vingine vya habari pia vimeripoti kwamba Rais Trump aliidhinisha mashambulizi hayo kujibu shambulizi liliofanywa na Iran kuangusha ndege isiyokuwa na rubani.

Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba serikali ya Iran imesema imepokea ujumbe kutoka kwa Rais Trump kupitia Oman, akiwaonya juu uwezekano wa mashambulizi dhidi ya nchi hiyo, hivi karibuni.

Reuters imesema jibu la papohapo kwa ujumbe wa Trump kutoka Tehran ni kuitahadharisha kuwa kutakuwa na maafa makubwa ya "kieneo na kimataifa" iwapo Marekani itachukua hatua zozote za kijeshi dhidi ya Iran

Udhibiti wa anga wa serikali kuu ya Marekani, walitoa amri Alhamisi jioni, ya kuzuia ndege za Marekani kuingia anga ya sehemu za Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman, kanda ambayo ndege isiyo na rubani ya Marekani iliangushwa na Iran.

Mashirika kadhaa ya ndege ya kimataifa, ikiwemo KLM ya Uholanzi na Qantas ya Australia, yanasema hayatarusha ndege zake juu ya anga ya Hormuz.

Ndege isiyo na rubani ya Marekani, ilikuwa inapaa katika anga ya Hormuz, ilipopigwa na kombora la Iran, tukio ambalo Trump amelieleza kuwa ni kitendo kibaya sana.