Kutokana na sintofahamu iliyokuwa imegubika fedha zilizotumika kutengenezea filamu ya Royal Tour nchini Tanzania, muongozaji wa filamu hiyo ambaye ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema fedha zote zilizokusanywa zimetumika katika sinema hiyo yenye lengo la kutangaza vivutio vya kitalii nchini.
Rais Samia akizungumza katika uzinduzi wa filamu hiyo Jumapili Mei 8, jijini Dar es salaam ameweka wazi kuwa fedha zilizotumika kuilipa kampuni iliyofanya filamu hiyo ni shilingi bilioni 7.
"Kulikuwa kuna hoja kadhaa kuhusu matumizi ya fedha, nataka nikiri kwenu kwamba fedha yote tuliyokusanya ndiyo iliyotumika kwenye Royal Tour, na tulitumia shilingi bilioni 7 kuliipa kampuni iliyofanya shooting na kutengeneza filamu nyingine" amesema Rais Samia.
"Juni 26 mwaka jana, nilifanya kikao cha 12 cha baraza la biashara Tanzania na niliwaomba wana baraza waniunge mkono katika mradi huu, na tarehe 23 Agosti mwaka jana niliandaa chakula cha hisani usiku na kuwaita wale wote walioahidi kuniunga mkono waje kuchangia, na michango ilikwenda vizuri" amesema Rais Samia.
Aidha amesema lengo lilikuwa kukusanya bilioni 20 lakini kwa uwezo wa Mungu alipata ahadi za bilioni 19 na milioni 39, ambapo pia jumla ya makusanyo ilikuwa ni bilioni 12 na milioni 759.
Pamoja na hayo Rais Samia ameahidi ujio wa sehemu ya pili na ya tatu ya filamu hiyo ili kuendelea kuitangaza Tanzania
"Nataka niwahakikishie bado tuna backup, Royal Tour phase one ndio hii tunaiona lakini walichukua picha nyingi sana, kwahiyo bado tutakwenda na phase two na phase three, kwahiyo fedha hii tuliyonayo tunakwenda kudevelop phase two na three ya Royal Tour" Rais Samia .
Filamu hiyo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwezi April mwaka huu nchini Marekani kabla ya kuzinduliwa Tanzania katika mikoa ya Arusha,Zanzibar na Dar es Salaam.