Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 22:36

Ongezeko la Mishahara Mei Mosi: Rais Samia awaacha njia panda wafanyakazi


Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaacha njia panda wafanyakazi wa taifa hilo la Afrika Mashariki katika nyongeza ya mshahara kwa kutotaja ni kiwango gani cha mishahara kitaongezeka.

Licha ya ahadi hiyo ya nyongeza amesisitiza kuwa hali ya uchumi si nzuri. Alibaini hayo wakati wa sherehe za sikukuu ya wafanyakazi Mei Mosi.

‘’Nimeagiza jambo liwepo (nyongeza ya mishahara) mahesabu yanaendelea tutajua lipo kwa kiasi gani ila siyo kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA kwa sababu mnajua hali ya nchi yetu na hali ya uchumi wa dunia sio nzuri sana,’’ alisema Rais Samia.

Wakiongea mara baada ya hotuba ya Rais baadhi ya wafanyakazi wamekuwa na maoni tofauti juu ya kauli hiyo huku wengine wakisema ni vizuri kutotaja lakini wengine wakiwa na wasiwasi huenda kiasi cha nyongeza ni kidogo.

‘’Unajua mama (Rais) ameongeza kimya kimya ili kuzuia mfumuko wa bei kwani wafanyabiashara huongeza bei za bidhaa wanaposikia kiasi kilichoongezwa,” amesema Mwalimu Ally Tenga.

‘’Kauli ya Rais inaonyesha kiwango alichoongeza kwenye mshahara ni kidogo ndiyo maana ameshindwa kukitaja hadharani na ameshatoa sababu kuwa uchumi wa nchi umeshuka,” amesema Anitha Paul

Awali Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Heri Nkunda akiongea kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani amesema kwa miaka miaka kadhaa wafanyakazi wa sekta binafasi na serikalini hawajaongezwa huku gharama za maisha zikiendelea kupanda siku hadi siku.

‘’Gharama za maisha zimezidi ile hali stahiki na ujira kwa wafanyakazi umeendelea kuwa duni,kwani kima cha chini cha mishahara kimeendelea kuwa duni ikilinganishwa na gharama za maisha kupanda na haziendani na viwango vya mishahara iliopo.”

TUCTA walipendekeza kima cha chini cha mshahara kiwe millioni moja na elfu kumi (1,010,000) ambayo itaendana na uhalisia wa maisha ulivyo hivi sasa.

Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi nchini Tanzania ‘’mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ndio kilio chetu,kazi iendelee’’.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Amri Ramadhani, Tanzania

XS
SM
MD
LG