Wizara ya mambo ya nchi za nje ilisema katika taarifa yake kwamba "imepokea kwa masikitiko makubwa" mauaji ya raia wake yaliyotokea katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika.
Waziri Christophe Lutundula alisema kuna dalili kwamba mashambulizi hayo ya anga "yalifanywa na jeshi la anga kwenye eneo linalokaliwa na wakazi wasio na silaha, wakiwemo raia wa kigeni. Katika shambulio hilo baadhi yao walijeruhiwa vibaya".
Waziri huyo alisema serikali inasubiri maafisa wa Sudan kutoa taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Khartoum imejikuta katika mapigano kati ya jeshi na kikosi cha dharura Rapid Support Forces (RSF) tangu tarehe 15 Aprili, huku raia wakijikuta kati kati ya mapigano hayo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetoa wito wa kuwepo na njia kuwaruhusu kuondoka raia wake waliojeruhiwa na wengine ambao bado wamekwama mjini Khartoum.
Pande zinazopigana zilifanya mashambulizi kutoka angani na ardhini katika mji huo mkuu siku ya Jumanne, na kuongeza ghasia na kuenea uvunjaji wa sheria unaowaongezea masaibu wakazi ambao tayari wanahangaikana na uhaba wa chakula na dawa.
Mapigano kati ya jeshi na kikosi cha RSF, sasa yameingia wiki yake ya nane, mapigano hayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia, na watu 400,000 kuvuka mipaka wakikimbia vita na zaidi ya watu milioni 1.2 kuuhama mji huo mkuu kwenda miji mingine.
Taarifa hii inatoka shirika la habari la Reuters