Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:38

Waliobaki Khartoum ni masikini


Watu wakimpita mwanamume aliyeendesha mkokoteni unaosukumwa na punda huko kusini mwa jiji la Khartoum, tarehe 1 Juni 2023. Picha na AFP.
Watu wakimpita mwanamume aliyeendesha mkokoteni unaosukumwa na punda huko kusini mwa jiji la Khartoum, tarehe 1 Juni 2023. Picha na AFP.

Wakati wakazi wa jiji la Khartoum wakitumia nyakati za utulivu kulikimbia jiji jilo, baadhi yao wanashindwa kugharamia safari ndefu, hatari na zenye usumbufu mkubwa kwenda nchi jirani kujiepusha na vita vya majenerali waliohasimiana, kutokana na kupanda kwa gharama za usafiri.

Wakiongea na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, wakazi waliobaki mjini Khartoum na wale walioweza kujitosa na kuukimbia mji huo na maeneo jirani, walisema gharama za safari ni kikwazo kwa wenye uwezo mdogo kifedha, na hivyo wanashindwa kuondoka kwenda maeneo salama ndani na nje ya nchi.

Wakazi ya Khartoum waliokwenda Misri waliiambia Sauti ya Amerika kuwa gharama za usafiri kutoka Khartoum kwenda Halfa, mji ulio mpakani mwa Sudan na Misri ni kati ya dola 300 mpaka 1000 au zaidi kwa kila abiria.

Safari inaweza kuchukua kati ya siku mbili mpaka wiki moja.

“ukitaka kuondoka unahitaji uwe na kitita cha pesa kwa nchi zote tatu, hususani ukitaka kuigharamia familia nzima” alisema mkazi mmoja aliyebaki mjini Khartoum.

Watu wanaokimbia ghasia, wakipakia mizigo yao kwenye basi huko Khartoum, tarehe 30 Mei 2023.
Watu wanaokimbia ghasia, wakipakia mizigo yao kwenye basi huko Khartoum, tarehe 30 Mei 2023.

Baadhi ya wale walioweza kwenda Misri walisema walilazimika kuunganisa safari kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kutumia usafiri wa mabasi boti na treni na sehemu nyingine kulazimika kutumia njia mbovu za vichochoroni na wakati mwingine kusimamishwa na vikosi vya RSF na kufanyiwa ukaguzi wa mizigo wa mara kwa mara.

Waliosafiri mwanzoni mara baada ya vita kuzuka, waliweza kuendesha magari yao binafsi , lakini sasa “watu wanaogopa kuendesha magari yao wakihofiwa kuporwa” alisema mkazi mmoja mjini Khartoum.

Mbali na kuhofia gharama za usafiri, waliosalia wamejikuta wakiwa wamenasa katika mji huo ulioharibiwa na vita na kuna ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu pamoja wizi, ubakaji, uharibifu wa mali na baadhi ya watu kutumiwa kama ngao.

“Tuko kwenye hali mbaya. Wanawake wanabakwa, wanaume wanadhaniwa na kuhusishwa na makundi yanayozozana na kuwa hatarini kupigwa risasi” alisema mkazi mwingine mjini Kartoum.

Wakazi wa Khartoum wakinunua vyakula wakati mapigano yalipositishwa, tarehe 31 Mei.
Wakazi wa Khartoum wakinunua vyakula wakati mapigano yalipositishwa, tarehe 31 Mei.

Wakazi hao wanaokabiliwa na ukosefu wa maji chakula , umeme na mawasiliano ya simu pia wamesema wamekuwa wakishambuliwa na wahuni.

“Kama ukitoka nje ya nyumba yako ina maana kuwa unaweza kupoteza kila kitu ndani ya nyumba.” alisema mkazi huyo.

“Majengo ya serikali na taasisi zenye nyaraka za kihistoria, vituo vya Sanaa na minara ya kihistoria imeibiwa” amesema mmoja wa wakazi wa Khartoum ambaye wiki iliyopita yeye na familia yake waliweza kuondoka Khatoum kwenda Kassala, mji uliopo kilometa 400 kutoka Khartoum.

MARIAM MNIGA, SAUTI YA AMERIKA, WASHINGTON DC.

Forum

XS
SM
MD
LG