Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa kufunga kikao maalum cha viongozi wakuu wa chama cha NRM kilichofanyika katika Wilaya ya Nwoya baada ya muswada uliyowasilishwa na kiranja wa serikali Ruth Nankabirwa na kukubaliwa na kamati nzima.
Kwa mujibu wa maamuzi ya kamati ya juu ya chama cha NRM, namba 1(g), viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho ambacho kimetawala Uganda tangu mwaka 1986, wamemuidhinisha Museveni kuitawala Uganda maisha yake yote.
NRM yamsifia Museveni
Wamemtaja kama kiongozi shupavu na Jenerali katika ukombozi wa Bara la Afrika, mwenye uwezo wa kuleta maendeleo ya kudumu, sio tu kwa Uganda na Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee, bali katika bara la Afrika kwa jumla.
kipengele namba sita cha taarifa iliyotolewa na meneja wa mawasiliano wa NRM Rodgers Mulindwa, kinasema kwamba uongozi wa NRM, umekubaliana kwamba Museveni atawania urais mwaka 2021 na katika chaguzi zitakazofuatia, wakati chama kinapoondoa changamoto za maendeleo nchini humo.
Kamati ya juu ya NRM imezingatia rekodi ya kisiasa na kiuchumi ya Museveni mwenye umri wa miaka 74, ndani ya Uganda, juhudi za kidiplomasia na majirani wa Uganda, Afrika mashariki na Afrika kwa jumla kabla ya kumuidhinisha, bila yeyote kati yao kupinga.
Wafuasi na wabunge wa NRM wamefurahia hatua hiyo. Henry Makumbi, Mbunge wa JImbo la Mityana kusini (NRM) amesema :
"Nafikiri hatua iliyochukuliwa na kamati kuu cha chama ni nzuri kulingana na mazingira tuliyonayo sasa kwa kuzingatia historia, yanayofanyika sasa na yanayoweza kujiri. Mzee ndiyo mtu pekee anayeweza kuweka mambo sawa na muda utakapowadia, atatupatia mtu anayefaa.
Alichosema Museveni
Kabla ya kuidhinishwa, Museveni, alikuwa amewahutubia wanachama wake kuhusu masuala ya ya siasa na uchumi. Alitumia pia Bibilia katika hotuba yake ya kufunga kikao hicho na kueleza ndoto yake ya kuistawisha jumuiya ya Afrika mashariki, hatua wanachama wake wanaamini Museveni ndiye kiongozi pekee nchini Uganda anayeweza kuitawala nchi hiyo kwa mda wa miaka 50 ijayo.
Wachambuzi wa siasa za Uganda kama Nabende Wamoto, wanamtazamo kwamba upinzani wa Uganda umegawanyika na hauwezi kumshinda Museveni katika uchaguzi.
Wamoto anaeleza : “watu wengi Zaidi wamekata tamaa kwa hivi vyama vya upinzani vya zamani. Matumanini yao yote wameyaweka kwa jina Bobi Wine. Kijana naye anaonekana amewasoma hawa wapinzani na kupata ujuahi kidogo kutoka kwa rais Yoweri Museveni. Anajipanga kwa usiri sana na nafikiri huo usiri ndio unamfanya hasa rais Yoweri Museveni kuogopa Zaidi."
Hatua ya mwisho
Hatua ya kuidhinishwa Museveni kuwa rais wa maisha hata hivyo inasubiri maamuzi ya kongamano kuu la chama mwezi Novemba mwaka huu, lakini wachambuzi wanadai kuwa kwa kawaida, hakuna atakayepinga.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016, kamati kuu ya NRM ilimuidhinisha Museveni kama mgombea pekee wa urais, na aliyekuwa waziri mkuu Amama Mbabazi alipoonyesha kupinga uamuzi huo, alifukuzwa katika chama, kufutwa kazi ya waziri mkuu na kuvuliwa cheo cha katibu mkuu wa chama.
Kulingana na katiba ya Uganda, Museveni anaruhusiwa kuwania urais bila kizuizi chochote, baada ya bunge kufanyia katiba marekebisho na kuondoa kizuizi cha umri kwa wagombea wa urais, mwaka 2017.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington DC