Hong Kong : Mtendaji mkuu wa serikali aondosha muswada bungeni

Wananchi wa Hong Kong wakimuangalia Mtendaji Mkuu wa serikali ya Hong Kong Carrie Lam akitangaza kuondoa muswada wenye utata bungeni Hong Kong, Jumatano, Sept. 4, 2019.

Mtendaji mkuu wa serikali ya Hong Kong Carrie Lam amesema serikali itaondoa rasmi muswada wa kuwahamisha washukiwa wa uhalifu kutoka Hong Kong kwenda China bara uliosababisha maandamano ya kuunga mkono demokrasia yaliyoendelea kuwa aghlabu na vurugu.

Katika ujumbe uliyotolewa na ofisi yake katika picha ya video Jumatano, Lam amesema anaondosha muswada huo, ambao ungeruhusu washukiwa wa uhalifu kupelekwa China bara kushtakiwa katika mahakama zake zinazodhibitiwa na Chama tawala cha Kikomunisti, "kuondoa wasiwasi ulioenea katika umma."

Lam ameusitisha muswada huo wakati maandamano yakiongezeka hapo mwezi wa awali, lakini alipuuzia wito wa kuuondosha kabisa bungeni. Katika uamuzi huo wa kushangaza Jumatano, Lam alikubali kutekeleza moja kati ya madai matano ya waandamanaji, ikiwemo tume huru ya kuchunguza madai ya ukatili uliofanywa na polisi na lengo la muda mrefu la kuwepo demokrasia zaidi katika eneo linalodhibitiwa na China.

Maandamano hayo yamekaribia kusimamisha maisha ya kila siku ya kituo hicho cha Asia cha kibiashara, ambapo waandamanaji wanavuruga shughuli za usafiri wa jiji hilo na viwanja vya ndege. Mamia, kama siyo maelfu ya waandamanaji wamekamatwa baada ya kukabiliana na polisi ambao wanatumia virungu na kuwarushia mabomu ya machozi na maji yanayoruka kwa kasi.

Lakini mwanademokrasia mkongwe wa Hong Kong Joshua Wong amewaambia waandishi baada ya tamko la Lam kuwa uamuzi wa kuondoa muswada huo ni “mabadiliko madogo sana, na umechelewa sana.”

Tangazo hilo la Jumatano limekuja siku kadhaa baada ya Lam aliposikika katika sauti iliyorikodiwa na kuhodhiwa na shirika la habari la Reuters akiwaambia viongozi wa biashara wa Hong Kong kwamba alisababisha “mgogoro mkubwa” wakati alipopeleka muswada wenye utata unaotaka kuwahamisha washukiwa wa uhalifu uliopelekea maandamano.

Katika sauti hiyo iliyorikodiwa, ambayo inapatikana katika mtandao [[https://www.scmp.com/video/hong-kong/3025554/leaked-audio-recording-hong-kong-leader-carrie-lam-appears-say-she-would]], analiambia kundi hilo la wafanyabiashara, “ Iwapo ninaweza kuchagua, kitu cha kwanza ni kujiuzulu, kuomba msamaha wa kweli ni kuwa nijiuzulu.”