Mkutano Mkuu wa UNGA kuanza Jumatatu ukigubikwa na mazishi ya Malkia Elizabeth

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa viongozi kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaanza wiki ijayo ukigubikwa na mazishi ya Malkia Elizabeth na wakati vita vya Ukraine vikielekea kuingia katika kipindi ambacho kinaweza kuwa muhimu sana.

Katibu Mkuu wa UN Antonia Guterres hatahudhuria mazishi ya Malkia ili aweze kuwepo New York kusimamia mkutano wa viongozi kuhusu Elimu Jumatatu.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres

Baada ya hapo atahudhuria ufunguzi wa mjadala wa kila mwaka Jumanne asubuhi, akiwaambia waandishi itakuwa “ni muhali” yeye kutokuwepo katika majadiliano hayo.”

Rais wa Marekani Joe Biden ambaye ndio kiongozi mwenyeji kwa kawaida anakuwa mkuu wa nchi wa pili kulihutubia baraza hilo Jumanne, lakini kwa kuwa atakuwa anahudhuria mazishi ya Elizabeth Jumatatu, maafisa wa Marekani wanasema siku ya kutoa hotuba yake imebadilishwa hadi Jumatano.

Wote Rais wa Russia Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy hawatahudhuria mkutano mjini New York, lakini juu ya hivyo, mvutano wao utatawala kwenye agenda ya mkutano wa mwaka huu.

Kushoto, Rais Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.

“Nafikiri kuwa Joe Biden na viognozi wengine wa Magharibi watatumia hili kama ni fursa ya kufikisha ujumbe juu ya hasira zao kwa Russia kutokana na vita hii,” Richard Gowan, mkurugenzi wa UN anayesimamia Kikundi cha Kimataifa kinachoshughulikia Migogoro, ameiambia VOA.

Amesema viongozi wa Magharibi pia watataka kuonyesha uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi ambazo wanahisi wanajaribu kuepuka kuonyesha wanaiunga mkono au wanaikosoa Russia.

Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield amewaambia waandishi Ijumaa kuwa uvamizi wa Russia nchini Ukraine “ni mtihani mkubwa kwa misingi mikuu ambayo iliifanya Umoja wa Mataifa uwepo.” Ameihimiza jumuiya ya kimataifa kutopuuzia misingi hiyo.

Balozi wa Marekani katika UN Linda Thomas-Greenfield

“Ni lazima tuongeze mara mbili ahadi zetu kufikia dunia yenye amani na hata tushikamane kwa karibu nguzo zetu zilizojikita katika haki ya kujitawala, kuheshimu mipaka, amani na usalama,” alisema.

“Na kwa sababu hii ndio maana wiki ijayo ni muhimu. Tunaamini hii ni fursa ya kuilinda Umoja wa Mataifa na kuonyesha kwa walimwengu kuwa inaweza kusimamia changamoto zenye shinikizo zaidi za dunia.”

Siku ya Alhamisi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa ngazi ya mawaziri kuhusu hali hiyo; kunaweza kutokea malumbano makali kati ya maafisa wa Russia na nchi za Magharibi. Kutakuwa pia na shughuli pembeni ya mkutano huo siku hiyo kuhusu kuwajibika kwa uhalifu wa kivita uliofanyika Ukraine.