Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linapanga kutoa msaada wa chakula unaowalenga watu 700,000 nchini Zimbabwe kuanzia Oktoba huku athari za mavuno duni na vita vya Ukraine vikiendelea kuonekana, afisa mmoja amesema.
Serikali ya Zimbabwe inafanya kazi na mashirika ya msaada ili kutoa chakula kwa watu milioni 3.8, WFP ilisema.
Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imekuwa ikijitahidi kujilisha tangu mwaka 2000, wakati kiongozi wa zamani Robert Mugabe alipotetea unyakuzi wa mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na wazungu ili kuwapa makazi watu weusi wasio na ardhi.
Serikali ya Zimbabwe imesema inatarajia mavuno ya zao lake kuu la mahindi kupungua kwa karibu nusu mwaka huu, hadi tani milioni 1.56 kutoka rekodi ya msimu uliopita ya tani milioni 2.72, kutokana na mvua duni katika msimu wa kilimo wa 2021-22.
Nchi inahitaji tani milioni 2.2 za mahindi kila mwaka kwa matumizi ya binadamu na mifugo.