Masoko ya China, Marekani yaathiriwa na mvutano wa ushuru

Mfugaji wa nguruwe Bruce Wessling katika shamba la nguruwe, Iowa, Marekani, Julai 5, 2018.

Wakati Marekani imeongeza ushuru kutoka asilimia 10 hadi 25 katika bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 200 zinazoingizwa kutoka China, kwa upande wake China imeongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazoletwa kutoka Marekani,

Pamoja na kuwepo mvutano huu wa kibiashara China haijaingia kwenye hali ya kulipiza kisasi. Badala yake, China imeonyesha ubabe wake kwa namna tofauti.

China yapunguza ununuzi

Katika hali iliyokuwa haijatarajiwa, China imepunguza kiwango cha bidhaa zinazoingizwa kutoka Marekani kwa kiwango cha dola za Marekani bilioni 6.5, na kuathiri vibaya sana wafugaji wa nguruwe wa Marekani ilivyokuwa China ndiyo ya pili inayoagiza kiwango kikubwa cha nguruwe kutoka Marekani.

Wachache walitegemea China kuchukua hatua hii wakati ambapo mifugo ya nguruwe ya China imekumbwa na mafua ya nguruwe. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa wafugaji wa nguruwe wako hatarini kupoteza thuluthi ya mifugo yao.

Wasemavyo wachambuzi

Wachambuzi wanasema China inawepesi mmoja ambao ni uwezo wake wa kuwafanya wananchi kufuata kile ambacho serikali inakitaka, hata kama ikimaanisha kupunguza manunuzi ya bidhaa zilizowekewa ushuru wa hali ya juu.

“China haihitaji kupunguza mahitaji yake kutokana na bidhaa zinazoingizwa kwa kulipia ushuru,” amesema Doug Barry, mtendaji mmoja anayefanya kazi katika Baraza la Biashara la Marekani na China. “Kwa urahisi kabisa inaweza kuelekeza kuwa manunuzi yote yasimamishwe.”

Soko la ajira mashakani

Katikati ya mvutano huu wa kibiashara, idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu milioni 8.34 wanatarajiwa kuingia katika soko la ajira katika kipindi hiki cha msimu wa joto.

Hili limefanya hali kuwa mbaya zaidi, kutokana na idadi ya nafasi za ajira nchini China kupungua wakati China ikijaribu kuondokana na viwanda vinavyo ajiri wafanyakazi zaidi.

Ajira nyingi zimechukuliwa na mashine aina ya roboti zinazofanya kazi zilizokuwa zinafanywa na binadamu, jambo linalowaathiri wale wanaotafuta ajira.