Kiongozi huyo anaonekana akichukua hatua hiyo ili kuondoa wasiwasi miongoni mwa nchi zinazoshiriki katika mradi wake mkubwa wa miundombinu wa ujenzi wa barabara na reli unaofahamika kama Belt and Road.
Akiizungumza katika mkutano wa pili wa kilele wa Belt and Road unaofanyika mjini Bejing na kuhudhuriwa na viongozi wapatao 47 na wajumbe 150 kutoka nchi mbali mbali, Xi alirejelea ahadi yake ya awali ya kupunguza ushuru, kuongeza ununuzi wa bidhaa kutoka nje ya China, kufanya msako dhidi ya wizi wa haki miliki na kufungua sekta kadhaa za uchumi wa China kwa wawekezaji.
Jinping ameonekana kutatua masharti muhimu ya Marekani, kabla ya mazungumzo kuhusu vita vya kibiashara, yanayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Marekani na China; nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, zinaonekana kukaribia makubaliano ya kibiashara yatakayo suluhisha mgogoro wa miezi kadhaa ambao umepelekea kuwekeana nyongeza ya ushuru wa zaidi ya dola bilioni 360 kwa bidhaa zake.
Mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer, na Waziri wa Biashara Steven Mnuchin, wanatarajiwa Beijing, April 30 kwa awamu nyingine ya mazungumzo, kabla ya mazungumzo zaidi kufanyika mjini Washington, mwezi Mei.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.