Gazeti la The East Africa linafahamu kuwa nchi tano kati ya sita wanachama wa EAC – ikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda na Sudan Kusini – ziko tayari kupeleka majeshi huko mashariki mwa DRC lakini zimesisitiza kuwepo kwa kanuni sahihi ili kuepuka makosa yaliyotokea katika vikosi vya awali vya kulinda amani.
Mkataba wa Majeshi na Kanuni za Mapambano ndiyo zitaangalia ukubwa, eneo la operesheni na mapambano huru kwa kila nchi inayochangia wanajeshi wake.
Viongozi wa EAC mwezi Juni walikubaliana kupeleka wanaajeshi “haraka” huko mashariki mwa DRC kama sehemu ya mpango wa kikanda ili kumsaidia mwanachama mpya wa jumuiya hiyo kupambana na waasi.
Chanzo katika Wizara ya Ulinzi mjini Nairobi kimesema Kenya iko tayari kupeleka wanajeshi mara tu mkataba huo utakaposainiwa. Majeshi yake yanafanya mafunzo huko Isiolo, kiasi cha kilomita 400 kaskazini mwa Nairobi.
Wiki iliyopita Kenya ilipeleka kundi la pili la kikosi cha kukabiliana na hali ya dharura huko DRC. Hata hivyo vikosi vitafanya kazi chini ya tume ya kulinda amani ya UN inayojulikana kama Monusco. Maafisa mjini Nairobi walikataa kueleza idadi kamili ya vikosi hivyo lakini walisema ni “zaidi ya wanajeshi 200” wenye vyeo na wa kawaida walipelekwa.
Chanzo cha habari hii ni gazeti la "The East African" linalochapishwa Kenya