Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:57

Kenya imetuma wanajeshi kulinda amani mashariki mwa DRC


Wanajeshi wa Kenya wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa katika bustani ya uhuru Park Nairobi Oktoba 20, 2011
Wanajeshi wa Kenya wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa katika bustani ya uhuru Park Nairobi Oktoba 20, 2011

Kenya imetangaza kutuma kundi la pili la wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kama sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa – MONUSCO.

Wanajeshi hao wanaingia DRC kwa ajili ya kupambana na waasi mashariki mwa nchi ambao wamekuwa wakitekeleza mauaji na uharibifu wa mali na maisha ya watu kwa muda mrefu.

Zaidi ya wanajeshi 200 wa Kenya, wamepewa maelekezo ya mwisho kwenye kambi ya kijeshi ya Embakasi jijini Nairobi baada ya kufanya mafunzo ya miezi mitano.

Raia wa DRC wanataka wanajeshi wa Monusco kuondoka nchini humo

Wanajeshi wa Kenya wanaungana na wenzao wa Umoja wa Mataifa wakati kuna shinkizo kutoka kwa raia wa DRC kutaka wanajeshi hao kuondoka nchini humo.

Raia wa DRC wanadai kwamba wanajeshi wa MONUSCO wameshindwa kuwalinda na kukabiliana na makundi ya waasi, na kwamba mauaji ya raia yanaendelea licha ya wanajeshi hao kushika doria nchini humo.

Maandamano makubwa yamefanyika DRC kutaka wanajeshi wa MONUSCO kuondoka. Maandamano hayo yalipelekea vifo vya raia na uharibifu wa mali.

Kundi la pili la wanajeshi wa Kenya kuingia DRC

Kundi la kwanza la wanajeshi wa Kenya lilitumwa nchini humo Agosti mwaka jana.

Linashika doria katika sehemu za Mavivi, Beni, Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Huu ukiwa ni muendelezo wa wanajeshi wa Kenya kushiriki katika operesheni za kulinda amani katika mfumo wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1979

Serikali ya rais Uhuru Kenyatta inaeleza kuwa inatarajia wanajeshi wake watakaokuwa sehemu ya jeshi hilo la Umoja wa Mataifa, kuwalinda raia wa Congo na kuendelea kutafuta amani kwa mujibu wa kanuni na maadili ya Umoja wa Mataifa.

“Kwa muda wa miaka kadhaa, Kenya imekuwa ikituma wanajeshi wake kulinda amani katika nchi mbalimbali na wamesifiwa kwa kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia maadili. Mnapokwenda DRC, mlinde sifa ya Kenya kwa sababu sio kwamba mnaiwakilisha KDF pekee lakini pia nchi nzima,” amesema naibu wa mkuu wa majeshi ya Kenya Lt. Generali Francis Ogolla.

Makubaliano ya viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki

Hatua ya Kenya inajiri miezi michache baada ya marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kukubali kupeleka jeshi la kikanda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa lengo la kuharakisha juhudi zinazoendelea za kikanda za kufikia amani na usalama endelevu Mashariki mwa nchi hiyo.

Marais wa Jumuiya ya Afrika mashariki pia walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa mchakato wa uondoaji silaha kutoka mikononi mwa waasi, amri ya kusitishwa uhasama, sitisho la mapigano bila masharti, na kukomeshwa kwa matamshi ya chuki, vitisho vya mauaji ya halaiki na ndimi za uchochezi wa kisiasa.

Wanajeshi wa Burundi wameingia DRC

Burundi imetuma wanajeshi wake mashariki mwa DRC chini ya mpango huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Wanajeshi wetu wamepokelewa rasmi nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Wapo Congo kwa kazi rasmi,” alisema msemaji wa jeshi la Burundi Cl. Floribert Biyereke, Jumatatu wiki hii, katika mahojiano na shirika la habari la Associated press.

Msemaji wa jeshi la DRC Lt. Marc Elongo naye alithibitisha kwamba Burundi imetuma wanajeshi wake nchini Congo, na kusema kwamba “ makundi yote yenye silaha, ya ndani ya nchi na yanayotoka nje ya nchi yatakabiliwa kijeshi.”

Kuna zaidi ya makundi 100 ya waasi Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, kwenye mpaka na Rwanda pamoja na Uganda ambapo kuna utajiri mkubwa wa madini.

DRC na Rwanda zimeshutumiana kuhusu kuyasaidia makundi ya waasi

Kwa muda sasa mabishano kati ya DRC na Rwanda yamezidi huku Kinshasa ikiishutumu Kigali kwa kuunga mkono kufufuka kwa kundi la waasi la M23 Mashariki mwa DRC.

Rwanda imekanusha tuhuma hizo dhidi na kuishtumu DRC kwa kuunga mkono wapiganaji wa FDLR.

DRC imesema kwamba haitaki wanajeshi wa Rwanda kuwa sehemu ya kikosi cha jeshi la Jumuiya ya Afrika mashariki. Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema wkamba "hatujaomba mtu yeyote kwamba tupeleke wanajeshi wetu nchini DRC."

Wakati wa ziara yake nchini DRC na Rwanda, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, alisema kwamba kuna ushahidi kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

Blinken alimtaka rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kufanya mazungumzo kumaliza mapigano mashariki mwa DRC.

Mwishoni mwa mwezi Julai, rais wa Rwanda Paul Kagame, alilishtumu jeshi la MONUSCO akidai kwamba linashirikiana na jeshi la DRC, pamoja na waasi wa FDLR kupambana na waasi wa M23.

Kundi la waasi la Democratic forces for liberation of Rwanda - FDLR, linashutumiwa na serikali ya Rwanda kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi.

XS
SM
MD
LG