Video hiyo inaonyesha ndege ya kivita ya Russia aina ya Sukhoi Su-27 ikimwaga mafuta wakati ikiisogelea droni ya Marekani aina ya MQ-9 kwa nyuma na kuipitia kwa juu.
Katika sekunde moja Sukhoi Su-27 inaisogelea kwa namna ile ile, na inapoifikia droni hiyo, rekodi ya video hiyo iliyokuwa inachukuliwa inakatika wakati huo jeshi la Marekani linasema kuwa ndege ya kivita ya Russia inagongana na droni hiyo.
Picha ya mwisho inaonyesha video hiyo imerejea kurekodi na moja ya panga za droni hiyo imepinda.
Kutolewa kwa video hiyo kumekuja siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kuzungumza na mwenzake wa Russia kuhusu tukio hilo.
“Marekani itaendelea kuruka na kufanya operesheni zake mahali popote sheria za kimataifa zinaporuhusu kufanya hivyo, na ni juu ya Russia kuendesha ndege zake za kijeshi kwa usalama na kwa weledi,” Austin aliwaambia waandishi wa habari baada ya kutangaza kwamba alikuwa “amemaliza kuzungumza kwa simu” na waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa mazungumzo ya simu kufanyika kati ya viongozi hao wawili wa ulinzi tangu mwezi Oktoba, kulingana na maafisa.