Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:07

Ndege ya kivita ya Russia yagongana na droni ya Marekani eneo la maji ya kimataifa


Ndege ya jeshi la Marekani isiyokuwa na rubani aina ya US MQ-9
Ndege ya jeshi la Marekani isiyokuwa na rubani aina ya US MQ-9

Jeshi la Marekani limesema kuwa ndege ya kivita ya Russia iligongana Jumanne na ndege isiyokuwa na rubani aina ya droni ya upelelezi, tahadhari na kuweka mikakati ya ulinzi.

Ajali hiyo ilisababisha droni hiyo iliyokuwa inafanya operesheni zake katika anga ya kimataifa katika eneo la bahari ya Black Sea kuanguka.

Afisa wa jeshi la Marekani ameiambia VOA ndege hiyo isiyokuwa na rubani aina ya US MQ-9 mpaka sasa haijapatikana. Wizara ya ulinzi ya Russia imeilaumu droni hiyo kwa kusababisha ajali na ilisema kuwa ndege zake za kivita Su-27 hazikukabiliana na ndege hiyo ya Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Ned Price alisema Marekani inamwita kwa mashauri balozi wa Russia kuhusiana na tukio hilo.

“Tunawasiliana moja kwa moja na Warussia, na katika ngazi za juu, kupeleka malalamiko yetu makali kuhusu ukosefu wa usalama, kukosekana weledi wa kufuatilia droni hiyo, ambao umesababisha kuanguka kwa ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani.”

Ameongeza kuwa Balozi wa Marekani nchini Russia Lynne Tracy “ amefikisha ujumbe mzito kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia.

Rais wa Marekani Joe Biden alipewa muhtasari kuhusi tukio hilo, kulingana na msemaji wa White House John Kirby.

“Iwapo ujumbe huu [kutoka Russia] ni kuwa wanataka kuzuia au kutuvunja moyo kuruka na kuwa na operesheni zetu katika eneo la anga ya kimataifa huko bahari ya Black Sea, hivyo ujumbe huo utashindwa kwa sababu hilo halitatokea,” Kirby alisema akijibu swali la VOA.

“Tutaendelea kuruka na kufanya operesheni zeti katika anga za kimataifa juu ya eneo la maji ya kimataifa. Bahari ya Black Sea siyo mali ya taifa lolote na tutaendelea kufanya kile tunachotakiwa kufanya kwa ajili ya maslahi ya usalama wa kitaifa katika eneo hilo la ulimwengu.”

Kulingana na Kamandi ya Marekani Ulaya, inayosimamia operesheni za jeshi la Marekani Ulaya, ndege mbili za Russia aina ya Su-27 “zilimwaga mafuta hapo na kuruka mbele ya droni aina ya MQ-9 bila uangalifu, kufanya hivyo kimazingira siyo salama na pia ni kinyume cha weledi.”

XS
SM
MD
LG