Marekani yaahidi kuendeleza ushirikiano na Jumuiya ya Afrika Mashariki

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright (Kulia) alipokutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Liberate Mfumukeko mjini Arusha. Picha na Asiraji, VOASWAHILI.

Marekani imeahidi kuendeleza ushirikiano wake na Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia kusaidia nchi wanachama katika sekta za kilimo, nishati, mazingira, kukuza demokrasia na uwezeshaji kwa vijana. 

Hayo yamesema na balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright ambaye alikutana na katibu mkuu wa jumuiya hiyo Liberate Mfumukeko mjini Arusha na kuelezea azma ya utawala mpya wa Marekani unatarajia kuendelea na kuimarisha ushirikiano na taasisi hiyo.

Rais wa Marekani Joe Biden

Balozi Donald pia amewasilisha hati ya utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo na kusema lengo lake ni kuendelea kuona Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye umuhimu mkubwa inaendelea kukua sambamba na jumuiya nyingine za kikanda.

“Marekani imejitolea kuzisaidia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ili ziendelee kukuza uchumi na pia kuwa na utulivu wa kisiasa. Marekani pia imejitolea kushirikiana na Jumuiya nyingine za kikanda na kimataifa sambamba na Umoja wa Afrika,”alisema Balozi Wright .

Kwa upande wake katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Mfumukeko amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri unaoendelea kati ya Marekani na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kwa muda mrefu sasa nchi za EAC zimekuwa zikinufaika na misaada kutoka Marekani ambayo imekuwa ikisaidia sekta mbali mbali katika nchi wanachama. Katika mazungumzo yetu pia nimemweleza baadhi ya maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele kwenye uwezeshaji hasa sekta ya Afya,” alisema Balozi Mfumukeko.

Pia balozi Mfumukeko alimweleza Balozi Wright hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mchakato wa kuondoa vikwazo vya kibiashara kwenye Forodha kwa nchi wanachama na itifaki za Soko la Pamoja na pia kuelekea kwenye sarafu moja mchakato ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2024.za Jumuiya ya Afrika Mashariki