Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:58

Uongozi wa Biden waanza kuchukua hatua kupunguza uchafuzi wa hewa


Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden

Rais Joe Biden amesaini amri kadhaa za utendaji ili kupunguza uchafuzi wa hewa kutokana na mafuta, gesi na mkaa, katika juhudi zake za kukabliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Biden anasema anataka Marekani kwa mara nyingine tena kuongoza dunia katika ajenda ya hali ya hewa, ikiwa ni mabadiliko makubwa kutoka sera za aliyemtangulia.

Mwaka 2020 ulikuwa ni wa joto zaidi kuliko mwaka mwengine ule katika historia ya dunia, kutokana na hali ya kuongezeka kwa joto duniani kufuatana na takwimu za Idara ya Safari za Anga ya Marekani, NASA.

Akiwa na lengo la kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na mafuta, gesi na mkaa, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa Rais Biden amesema Marekani haiwezi tena kusubiri ili kukabiliana na janga la hali ya hewa duniani akiitaja kuwa ni tishio kubwa kabisa.

Rais Joe Biden aeleza : "Na sawa na jinsi tunavyo hitaji jibu la pamoja la kitaifa kukabiliana na Covid 19, tunahitaji kwa fharura jibu la pamoja la kitaifa kwa ajili ya mzozo wa hali ya hewa, kwa sababu kuna mzozo wa hali ya hewa. Ni lazima tuongoze dunia katika kukabiliana na janga hili."

Hapo jana jioni Rais Biden alisaini amri ya utendaji juu ya masuala ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kusitisha kutolewa vibali vipya vya uchimbaji mafuta na gesi na kumaliza ruzuku kwa ajili ya mafuta ghafi. Amri hiyo inachukuwa hatua ya kuhifadhi asilimia 30 ya ardhi ya nchi hii na maji kufikia 2030, na kuelekea katika kutumia magari ya serikali yenye nishati za umeme.

Hatua hii inafuatia hatua ya kwanza aliyochukuwa Biden alipoingia madarakani ya kuirudisha Marekani kwenye mkataba wa kimataifa wa kupambana na mabadliko ya hali ya Hewa, mkataba wa Paris ambao Rais wa zamani Donald Trump aliiondoa Marekani mwaka 2017.

John Kerry
John Kerry

Mjumbe maalum wa Rais Biden kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa John Kerry ana hisi mambo mengi zaidi yanabidi kufanyika.

John Kerry afafanua : "Mkataba wa Paris pekee hautoshi, wakati asilimia 90 ya uchafu wote wa hewa duniani unatokea nje ya mipaka ya Marekani. Tunaweza kufikia kiwango cha sifuri kesho lakini tatizo litakuwa halijatanzuliwa bado."

Kerry anasema utawala wa Biden utapendekeza uchunguzi ufanyike wa makadirio ya kitaifa juu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa usalama wa taifa. Na kwa mara ya kwanza kabisa, suala la mabadiliko ya hali ya hewa litachukuliwa kama msingi wa sera za usalama wa taifa na masuala ya kigeni ya Marekani.

Vishwas Satgar wa chuo kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini anasema changamoto itakuwa ni vipi Biden atapambana na maslahi ya makampuni husika.

Vishwas Satgar aeleza : "Mtihani utakuwa ni namna Biden atakavyo pambana na vizuizi, jinsi atakavyo ongoza agenda yake, na hata kukabiliana na maslahi yaliyo kita mizizi, huku akifanya kazi na wadau wa ndani ya Marekani na kimataifa, wenye dhamira ya kuondoa kabisa uchafu wa mkaa duniani.

Biden amesema mpango wake wa mabadiliko ya hali ya hewa utasaidia kuufufua uchumi kwa kubuni nafasi za ajira kwa wafanyakazi wa sekta inayoporomoka ya mafuta ghafi. Wazo linalo kosolewa vikali na wakuu wa vyama vya wafanyakazi wa mkaa.

Mpango wa utawala wa mabadiliko ya hali ya hewa unaweka pia kipau mbele cha haki ya usawa wa mazingira kukuzitaka idara za serikali kuwekeza katika jamii za mapato ya chin na wastani, zinazobeba mzigo mkubwa wa atahri za majanga asili, uchafuzi wa hali ya hewa na atahri nyenginezo.

XS
SM
MD
LG