Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 21:18

Viongozi duniani kuimarisha ushirikiano na uongozi wa Biden


Rais Joe Biden
Rais Joe Biden

Wanasiasa, viongozi na wananchi wa sehemu mbalimbali za dunia kwa upande wao kwa ujumla wamefurahia kuapishwa kwa Joe Biden kuwa Rais wa 46 wa Marekani pamoja na Makamu Rais wake Kamala Harris.

Mara tu baada ya kuapishwa Biden ameirudisha Marekani katika makubaliano ya Paris juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na kuanza kutoa amri za utendaji kubadili sera za ndani na kimataifa za aliyemtangulia Donald Trump.

Hatua ya kwanza aliyochukua rais mpya wa Marekani Joe BIden mara tu baada ya kuapishwa kwake Jumatano ni kuirudisha Marekani kwenye jumuia ya kimataifa kwa kutia saini amri ya utendaji ya kujiunga tena na mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Chansela wa Ujerumani Angele Merkel anasema anatarajia kufungua ukurasa mpya wa uhusiano na ushirikiano kati ya Ujerumani na Marekani.

Merkel anaeleza : "Kuna maelewano mpana zaidi kuhusu makubaliano ya kisiasa pamoja na Rais Biden, ukitizama amri za utendaji alizotia saini jana, unaweza kuona kwamba tunaweza kufanya kazi tena pamoja kuhusu WTO, Tunaweza kufanya kazi kuhusu makubaliano ya Paris, na hata pengine tunamtizamo sawa juu ya masuala ya uhamiaji."

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel kwenye ujumbe wa Twitter amewapongeza Biden na Harris akisema huu ni wakati wa kurudisha tena nguvu za fikra na kufufua uhusiano kati ya pande mbili.

China nayo imeeleza matumaini ya kurudisha uhusiano wa maelewano na maridhiano kati ya mataifa haya makuu ya dunia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa China Hua Chunying, amesema baada ya mivutano na matatizo wananchi wa Marekani na China wanastahiki mustakbal mzuri wa ushirikiano.

Chunying amesema : "Nimeona Rais Biden akitaja mara ningi neno umoja, na mimi ninadhani hilo bila shaka ni jambo ambalo uhusiano kati ya Marekani na China linahitaji."

Huko Mashariki ya Kati Israel imeeleza kwa wakati mmoja matumaini na wasiwasi, kutokana na kwamba utawala wa rais wa zamani Donald Trump ulitoa ushirikiano wa kipekee na mkubwa kwa Israel pekee yake.

Huku Utawala wa Biden umeahidi kuwa na mtizamo wa sawa kuhusina na Mashariki ya Kati na kurudisha msaada kwa Wapalestina na kufanya kazi kufufua mazungumzo ya amani.

Msemaji wa kundi la Hamas Hazem Qasem amesema ana matumiani utawala mpya utaanzisha njia mpya ya kisiasa katika kanda nzima na kurekebisha makosa ya kihistoria yaliyo fanyika dhidi ya Wapalestina.

Rais wa Iran Hassan Rouhani amefurahia kuondoka kwa Donald Trump na kurudi kwa utawala wa sheria kwenye White House.

Rouhani amesema : "Mpira hivi sasa uko upande wa Marekani. Ikiwa watarudi katika kufuata sheria sisi tutatekeleza ahadi zetu. Trump ameondoka na siasa zake zimekufa lakini mpango wa pamoja wa Iran, JCPOA, uko hai.

Viongozi wa nchi za Afrika kwa ujumla wameeleza katika ujumbe wao wa pongezi kuwa na matumaini ya kufunguliwa ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Marekani na bara la Afrika.

Waziri mteule wa Mambo ya nchi za nje wa utawala mpya Antony Blinken, akizungumza sku moja kabla ya kuapishwa kwa Biden amesema wanataka kufanya kazi na washirika wote kote duniani na kufufua diplomasia ya Marekani kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo hivi sasa.

XS
SM
MD
LG