Floyd, mtu ambaye kifo chake kimetokea akiwa ameshikiliwa na polisi kimepelekea maadamano ya zaidi ya wiki mmoja yakidai haki na mageuzi ya mifumo.
Kiongozi wa haki za kiraia Mchungaji Al Sharpton anaongoza ibada binafsi Alhamisi ilioandaliwa kwa ajili ya familia na marafiki wa marehemu.
“Inatukumbusha orodha ndefu ya wale waliouawa bila ya haki na polisi na wale waliouawa bila ya haki kwa sababu ya upendeleo, wasiokubali rai za wengine, na wabaguzi,” Sharpton amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii kabla ya ibada hiyo.
“Tunawafikiria wapendwa wao, tunafikiria wangekuwa nani. Tunafikiria michango yao ambayo wangeweza kuleta katika jamii, na hivyo tumenyanyuka na kuchukua hatua ili kufikia haki na usawa.”
Kuuaga mwili wa marehemu katika ibada ya umma na binafsi imepangwa kufanyika Jumamosi huko North Carolina, jimbo ambako Floyd alizaliwa, na itafuatiwa na ibada kubwa Jumatatu huko Houston ambako alikuwa kwa muda mwingi zaidi wakati wa uhai wake.
Waandamanaji wamepokea kwa moyo mkunjufu hatua ya waendesha mashtaka wa jimbo la Minnesota kuwafungulia mashtaka maafisa wengine watatu kuhusiana na kifo cha Floyd.
Maandamano siku ya Jumatano usiku katika miji mbalimbali kwa mara nyingine yalikuwa kwa kiwango kikubwa ya amani.
Mjini Washington, maelfu ya watu waliandamana nje ya White House na Bunge la Marekani, na kutembea kwenda mtaa wa Pennsylvania wakati Vikosi vya Taifa, polisi na walinzi kutoka vikosi vya serikali kuu wakilinda maeneo hayo.
Meya wa Washington Muriel Bowser alilegeza masharti ya kutotoka usiku, yakianza saa tano usiku badala ya saa moja usiku, baada ya usiku kadhaa wa utulivu.
Mkuu wa polisi huko Detroit amesema maafisa wa polisi hawatamzuia mtu yeyote atakaye andamana kwa amani baada ya sheria ya kutotoka usiku ilipoanza kutekelezwa, wakati Meya wa Seattle Jenny Durkan aliondoa amri ya kutotoka usiku ambayo ilitakiwa itekelezwe hadi Jumamosi.
Meya wa San Francisco London Breed na Meya wa Los Angeles Eric Garcetti wamesema wamepanga kusitisha amri ya kutotoka usiku Alhamisi.
Maandamano nchini Marekani yalianza huko Minneapolis, ambako Floyd, Marekani mweusi mwenye miaka 46, alifariki Mei 25 baada ya polisi wazungu kumshikilia chini ya ulinzi wakimlaza kifudifudi barabarani na mmoja wao kumkandamiza shigo yake kwa goti kwa dakika kadhaa.
Mwanasheria Mkuu wa Minnesota Keith Ellison alitangaza Jumatano kuwa Derek Chauvin, aliyemkamata Floyd, amefunguliwa mashtaka ya daraja la pili la mauaji na daraja la pili la mauaji bila ya kukusudia baada ya kukamatwa wiki iliyopita.
Ellison pia ametangaza kufunguliwa mashtaka ya kusaidia uhalifu huo na kushiriki katika daraja la pili la mauaji dhidi ya maafisa wengine watatu waliokuwa katika tukio la kukamatwa Floyd : J.A. Keung, Thomas Lane and Tou Thao. Maafisa wote wanne wamewekwa rumande na kufukuzwa kazi idara ya polisi.
“Naamini kuwa hatua hizi ni kwa maslahi ya Floyd katika kutendewa haki, familia yake na jamii yetu na jimbo letu,” Ellison amesema.
Tunashirikiana katika kesi hii kwa lengo moja tu : kuhakikisha George Floyd anatendewa haki.”
Wawakilishi Justin Amash na Ayanna Pressley wametangaza Jumatano kuwa wanaongoza muswada wa kufuta kinga ya polisi, kitu kitachofanya iwe rahisi watu waliodhulumiwa haki za kiraia kuwashtaki maafisa katika mahakama ya kiraia.
Kinga hiyo inazuia polisi kuwajibishwa, inazuia haki ya kweli kutendeka, na inazuia haki za kikatiba za kila mtu katika nchi hii,” Pressley amesema.
Katika moja ya taarifa chache za mapambano Jumatano usiku, polisi wa New Orleans walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji. Maafisa wa polisi wamesema waandamanaji walikaidi amri ya kutovuka daraja.